Amir Abdollahian nchini Lebanon; safari yenye malengo kadhaa
Hossein Amirabdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametembelea Beirut, mji mkuu wa Lebanon ikiwa ni katika muendelezo wa mashauriano yake na viongozi wa eneo kuhusu hujuma ya Wazayuni katika Ukanda wa Gaza ambapo amekukutana na kuzungumza na maafisa wa nchi hiyo pamoja na viongozi wa mrengo wa muqawama wa Lebanon na Palestina.
Takriban siku 50 zimepita tangu kuanza vita vya pande zote na vya kikatili vya utawala unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu dhidi ya Ukanda wa Gaza, vita ambavyo jinai zake ni mifano ya wazi ya ukiukaji wa sheria na mikataba ya kimataifa. Hadi sasa, juhudi nyingi za kidiplomasia zimefanywa na nchi za eneo la Asia Magharibi kwa lengo la kusimamisha vita hivyo vya kinyama dhidi ya watu wasio na hatia. Hossein Amirabdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa maafisa ambao pamoja na kufanya safari nyingi za nje ya nchi amelaani vikali jinai zinazofanywa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina na kusisitiza juu ya ulazima wa kuwepo makubaliano ya kieneo, Kiislamu na kimataifa kwa ajili ya kusimamisha vita hivyo.
Katika kuendeleza mashauriano hayo, Amir Abdollahian alielekea Beirut, mji mkuu wa Lebanon, siku ya Alkhamisi. Hiyo ni safari yake ya pili nchini Lebanon na ya tatu katika nchi za eneo tangu kuanza vita vya Gaza. Safari ya Amir Abdollahian nchini Lebanon na mazungumzo yake na viongozi wa nchi hiyo ni miongoni mwa hatua muhimu za kidiplomasia zinazofanyika kwa ajili ya kuwatetea watu wa Ghaza dhidi ya jinai za Wazayuni.
Ziara ya Amir Abdollahian nchini Lebanon ni muhimu kwa sababu Lebanon imehusika katika vita vya siku 50 zilizopita ambapo imekuwa ikitishwa mara kwa mara na Wazayuni. Ingawa Hizbullah ya Lebanon haishiriki katika vita hivyo kwa kiasi kikubwa, lakini imeondoa sehemu ya nguvu za kijeshi za Wazayuni huko Gaza kwa mashambulizi inayofanya katika maneo ya kijeshi ya utawala huo kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Katika kikao na viongozi wa kisiasa wa Hizbullah wakiongozwa na Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Hizbullah, Amir Abdollahian amesisitiza juu ya kuendelea uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa Lebanon.
Kwa hakika, kama ilivyo kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Lebanon nayo inaiunga mkono Palestina dhidi ya utawala wa Kizayuni. Kuhusiana na hilo, Najib Miqati, Waziri Mkuu wa Lebanon, amekosoa misimamo ya kundumakuwili ya baadhi ya nchi na mashirika ya kimataifa kuhusu matukio ya Gaza na kuhoji: "Swali la msingi ni kuwa je, haki za binadamu ziko wapi?" Amesema: "Lebanon imekuwa ikitetea suala la Palestina tangu maafa ya Nakba, miaka 75 iliyopita, kwa sababu tunachukulia Palestina kuwa suala la haki na mabavu hayapasi kuruhusiwa kuitawala haki."
Sababu nyingine ya umuhimu wa safari ya Amir Abdollahian nchini Lebanon ni kukutana kwake na maafisa wa muqawama wa Palestina. Akizungumza katika kikao na Ziad Nakhale, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina, na Khalil al-Hayya, Mkuu wa Mahusiano ya Kiarabu na Kiislamu na Makamu Mwenyekiti wa Harakati ya Hamas ndani ya Gaza, Amir Abdollahian ametuma salamu za rambirambi kwa familia za mashahidi zaidi ya 15,000 huko Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, na kuwatakia ahueni ya haraka na afya njema maelfu ya watu waliojeruhiwa kutokana na mashambulizi ya kiwendawazimu ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza na pia kuwapongeza kutokana na mafanikio na ushindi wa mrengo wa muqawama dhidi ya Wazayuni. Kikao cha Amir Abdollahian na viongozi wa muqawama wa Palestina ni muhimu sana kwa sababu kimefanyika katika mkesha wa kutekelezwa usitishaji vita kati ya Hamas na utawala wa Kizayuni, na bila shaka kinaonyesha uungaji mkono wa Iran kwa usitishaji vita huo.
Baada ya Lebanon, Amir Abdollahian ameelekea Qatar kwa lengo la kushauriana na viongozi wa nchi hiyo kuhusu haja ya kudumishwa usitishaji vita huko Gaza. Qatar imekuwa na nafasi muhimu katika makubaliano ya sasa ya kusitisha mapigano.