Vita vya Gaza na kushadidi matatizo ya kiuchumi ya Israel
Vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya ukanda wa Gaza vilisitishwa kwa muda baada ya takriban siku 50, katika hali ambayo, Tel Aviv imepata hasara kubwa za kiuchumi.
Yamkini utawala wa Kizayuni ukayachukulia mauaji ya halaiki huko Gaza kuwa ni ushindi kwake, lakini hapana shaka kuwa utawala huu haujapata ushindi wowote ule katika medani halisi ya vita. Sio tu kwamba, malengo yake ya kijeshi hayakufikiwa, lakini Israel ilipata hasara kubwa za kibinadamu na kiuchumi.
Kwa upande wa kiuchumi, Wizara ya Fedha ya utawala huo ilitangaza mwezi Oktoba kwamba gharama za kila siku za vita hivyo ni takriban dola milioni 270. Hii ina maana kwamba, kwa mwezi utawala huo ghasibu unatumia zaidi ya dola bilioni 8. Hii ni katika hali ambayo, bajeti iliyotangazwa ya kila mwaka ya Wizara ya Vita ni kama dola bilioni 24. Kwa maneno mengine ni kuwa, takriban dola bilioni 16, sawa na takriban asilimiia 70 ya bajeti ya kijeshi ya mwaka ya Israel, ilitumika katika kipindi cha siku 50 pekee.
Katika ripoti zingine, gharama za kiuchumi za vita zimetangazwa kuwa zilikuwa kubwa zaidi. Chaneli ya 12 ya Televisheni ya utawala wa Kizayuni iliripoti kuhusu kikao cha wakurugenzi waandamizi wa Wizara ya Fedha ya utawala huo na baraza la mawaziri kilichochukua muda wa saa 3 ambapo gharama za vita dhidi ya Gaza zilijadiliwa. Kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa katika mkutano huo, kila siku moja ya vita huugharimu utawala wa Kizayuni takribani shekel bilioni moja za Kiisrael, na hii ni pamoja na gharama za moja kwa moja za vita zikiwemo za malipo ya mishahara ya wanajeshi, kiasi kwamba, kila askari hulipwa shekel 1000 kwa siku. Mbali na hiyo kuna gharama za ndege kivita, mafuta na kudhamini chakula na vifaa vya kijeshi ni sehemu nyingine inayojumuisha kiasi hicho cha fedha.
Fauka ya hayo, vita hivyo vimesababisha pia nakisi ya bajeti ya Israel. Gazeti la Financial Times liliripoti kuwa nakisi ya bajeti ya Israeli itaongezeka mara tatu mwaka ujao (2024) na itafikia karibu asilimia 5-8 ya pato ghafi la taifa.
Benki Kuu ya utawala wa Kizayuni pia ilitangaza kuwa, mzigo wa gharama kwa uchumi wa utawala huo kutokana na ukosefu wa nguvukazi umefikia shekel bilioni 2.3 kwa wiki. Asasi hiyo ya Kizayuni imeongeza kuwa, gharama hizo zinatokana na kufungwa kwa shule nyingi katika maeneo tofauti ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na uhamisho wa wafanyakazi wapatao 144,000 kutoka maeneo ya karibu na mipaka ya Gaza na Lebanon, na pia kuitwa nguvukazi ya akiba kwa ajili ya kuhudumu jeshini.
Serikali ya utawala wa Kizayuni imewaita askari wake wa akiba 360,000 kwa ajili ya utumishi jeshini, ambapo hiki ni kiwango kikubwa zaidi katika historia ya utawala huo katika vita vyake vya huko nyuma dhidi ya Gaza, na hii imesababisha wafanyakazi wafanyakazi wengi kuondoka katika maeneo yao ya kazi.

Majimui ya mazingira haya yameufanya utawala wa Kizayuni uanze kufanya marekebisho ya bajeti ya mwaka huu wa 2023; jambo ambalo lenyewe limekuwa mahali pa mabishano na mivutano ya ndani ambayo kelele zake hazisikiki sana kutokana na anga ya sasa kutawaliiwa na habari za vita.
Matatizo ya kiuchumi ya utawala wa Kizayuni yameoongezeka kutokana na vita vya siku 50 katika hali ambayo, changamoto za kiuchumi zilikuwa moja ya sababu za kuenea malalamiko na maandamano ya wananchi kabla ya vita vya sasa, ambapo Waziri Mkuuu Benjamin Netanyahu alikuwa katika mashinikizo makubwa huku serikali yake ikikalia kuuti kavu.