Waandamanaji Uturuki: Marekani ndiye shetani halisi
(last modified Mon, 01 Jan 2024 11:55:02 GMT )
Jan 01, 2024 11:55 UTC
  • Waandamanaji Uturuki: Marekani ndiye shetani halisi

Kwa mara nyingine tena, wananchi wa Uturuki wamekusanyika nje ya Ubalozi Mdogo wa Marekani mjini Istanbul katika maandamano ya kuonyesha himaya na uungaji mkono wao kwa wananchi wa Palestina hususan wa Ukanda wa Gaza wanaoendelea kukabiliwa na hujuma na mashambulio ya kinyama ya utawala haramu wa Israel.

Waandamanaji hao, wakiwa wamebeba mabango na maberamu, wamelaani vikali jinai za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza. Wamesema Marekani ndiye shetani halisi na mvurugaji wa amani na usalama duniani.

Baadhi ya mabango yalikuwa na jumbe zinazosema: Tunalaani mshirika wa Israel katika jinai, yaani Marekani; Mlezi wa genge la Kizayuni, Marekani, ondoka Asia Magharibi.

Maandamano hayo ya jana Jumapili mjini Istanbul yamefanyika kufuatia mwito na kampeni zilizoongozwa na asasi zisizo za kiserikali za Kiislamu nchini humo.

Waandamanaji hao wamesema wataendelea kusimama na kuwaunga mkono wakazi wa Gaza, huku wakilaani misaada ya kifedha na kijeshi ya Marekani kwa utawala huo pandikizi unaoaendelea kuua wanawake na watoto wa Gaza.

Makumi ya maelfu ya Waturuki katika maandamano ya kuitetea Palestina

Maandamano ya mataifa ya Kiislamu wakiwemo wananchi Waislamu wa Uturuki dhidi ya jinai za Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu yanaendelea kushuhudiwa kila leo.

Kadhalika jana Jumapili, maandamano ya kuonyesha mshikamano na Wapalestina na kulaani jinai za kutisha za Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza yalifanyika mjini Berlin nchini Ujerumani na huko New York, Marekani.

Licha ya hujuma hizo za kutisha za Israel kupelekea kuuawa shahidi Wapalestina zaidi ya 22,000 huko Gaza tokea Oktoba 7, lakini nchi za Magharibi hasa Marekani na waitifaki wake bado zinaendeleza uungaji mkono wao kwa jinai hizo za Israel.