Kwa nini utawala wa Kizayuni unaitishia Lebanon mara kwa mara?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i107890-kwa_nini_utawala_wa_kizayuni_unaitishia_lebanon_mara_kwa_mara
Yoav Gallant, Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel meidai katika matamshi yake kuwa yaliyojiri Gaza huenda yakajikariri nchini Lebanon.
(last modified 2024-02-01T23:06:06+00:00 )
Feb 01, 2024 23:06 UTC
  • Kwa nini utawala wa Kizayuni unaitishia Lebanon mara kwa mara?

Yoav Gallant, Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel meidai katika matamshi yake kuwa yaliyojiri Gaza huenda yakajikariri nchini Lebanon.

Mwezi wa nne wa vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza unakaribia kumalizika. Katika kipindi hicho zaidi ya Wapalestina elfu 29 na 600 wa Gaza wameuawa shahidi na wengine karibu elfu 66 wamejeruhiwa.

Kimsingi Ukanda wa Gaza umepoteza muundo wake, na mauaji ya kimbari yanayojiri katika eneo hilo yameharibu miundombinu ya Gaza. Katika  siku za hivi karibuni baadhi ya viongozi wa Kizayuni wamekuwa wakionya mara kwa mara kuhusu uwezekano wa kufanya mashambulizi ya pande zote nchini Lebanon. Swali muhimu linalojitokeza hapa ni kuwa, kwa nini utawala haramu wa Israel unatilia mkazo kurudia tena unyama unaofanyika Gaza nchini Lebanon?

Benjamin Netanyahu

Sababu ya kwanza kuhusiana na suala hilo ni kuwa utawala ghasibu na katili wa Israel umepata kipigo kikubwa katika kipindi cha miezi minne iliyopita huko Kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na karibu na mipaka yake na Lebanon kutokana na mashambulizi ya wanamapambano wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon ambayo yameangamiza baadhi ya askari wake na kuutia hasara kubwa za kiuchumi utawala huo. Kwa hivyo kwa kutoa vitisho vya kuishambulia Lebanon, watawala wa Tel Aviv wanajaribu kusimamisha mashambulizi ya kaskazini ya wanamuqama au kufikisha ujumbe kwamba iwapo yataendelea, mapigano na utawala huo wa kimbavu yatakuwa na athari mbaya sana.

Sababu ya pili ni kuwa, Israel inafanya kila iwezecho kuonyesha sura yake halisi ya dola kichaa ambalo halisiti kufanya jinai na uhalifu wa aina zote ikiwa ni pamoja na mauaji ya kimbari ambayo yanapingwa na wanadamu huru. Kwa kujionyesha hivyo, utawala huo wa kibeberu unafanya jitihada za kuzuia vitisho vya baadaye na pia kutoa ujumbe kwa jamii ya Kimataifa kwamba hautishiki au kubabaishwa na maamuzi yao kama hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki.

Sababu ya tatu ni kwamba, utawala huo mpende vita umekata tamaa ya kufikia malengo yake ya kijeshi katika vita vya Gaza na unafanya jihada za mfa maji za kupanua vita hivyo katika eneo la Magharibi mwa Asia kwa kutoa vitisho dhidi ya Lebanon, na huenda hata ukafungua uwanja wa kuyaingiza madola ajinabi kwenye vita hivyo.

Biden na Netanyahu

Sababu ya nne ni kuwa, kwa kutoa vitisho dhidi ya Hizbullah au hata uwezekano wa kuanzisha vita dhidi ya Lebanon, Israel inajaribu kuyumbisha na kuteteresha nafasi ya harakati hiyo ya mapambano ndani ya Lebanon na kuchochea maoni ya wananchi dhidi ya harakati hiyo.

Nukta ya mwisho ni kwamba, baadhi ya Wazayuni wanaonya kuwa kuingia vitani na Lebanon si tu kwamba hakutakuwa na matokeo sawa na ya Gaza, bali kunaweza kuisababishia Israel madhara makubwa; kwa sababu kwa sasa Hizbullah imeanzisha vita vya kisaikolojia dhidi ya utawala huo ghasibu na bado haijaonyesha uwezo wake wote.