Guterres alaani hatua ya Israel kutumia Akili Mnemba (AI) vitani Gaza
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amekemea hatua ya utawala haramu wa Israel kutumia akili mnemba au Artificial Intelligence (AI) kwenye vita dhidi ya raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.
Akizungumza na waandishi habari Ijumaa New York huku vita vya mauaji ya kimbari vya utawala haramu wa Israel dhidi ya Gaza vikiwa vitamiza miezi sita kesho, Guterres amerejelea wito wake wa sitisho la mapigano kwa misinigi ya kiutu, kuachiliwa kwa mateka wote bila masharti, ulinzi wa raia na misaada ya kiutu ifikie walengwa bila vikwazo vyovyote.
Akiashiria ziara yake ya hivi karibuni kwenye kivuko cha Rafah ambako anasema alikutana na wafanyakazi wa kutoa misaada ya kibinadamu walimueleza wazi kuwa janga la Gaza si la kawaida na hawajawahi kushuhudia kokote.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema amechukizwa na kitendo cha Israel kutumia Akili Mnemba vitani Gaza hasa kwenye maeneo yenye watu wengi. Amesisitiza kuwa Akili Mnemba inapaswa kutumika kwa manufaa na sio kuchangia kwenye kuendeleza vita. Wataalamu wanasema matumizi ya akili mnemba vitani Gaza ni chanzo cha kuuawa kiholela idadi kubwa ya raia, hasa wanawake na watoto
Amekumbusha kuwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia na waandishi wa habari nao wameuawa kwenye vita vya Israel dhidi ya Gaza.
Utawala katili wa Israel ulianzisha vita vyake vya mauaji ya halaiki huko Gaza tarehe 7 Oktoba baada ya kundi la muqawama la Hamas la Palestina kutekeleza Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa dhidi ya utawala ghasibu wa Isarel ili kulipiza kisasi kwa ukatili wa utawala huo dhidi ya watu wa Palestina.
Tangu kuanza kwa mashambulizi hayo, utawala wa Tel Aviv umeua Wapalestina zaidi ya 33,100 na kuwajeruhi wengine karibu 75,750, wengi wakiwa ni wanawake na watoto.