UNRWA: Asilimia 62 ya nyumba Gaza zimeharibiwa katika mashambulizi ya Israel
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina limesema, vita vinavyoendelea vya Israel dhidi ya Gaza vimeacha zaidi ya asilimia 60 ya nyumba katika eneo hilo lililozingirwa ama kuharibiwa au kubomolewa kikamilifu.
"Mgogoro unaoendelea umeharibu au kubomoa kikamilifu takriban asilimia 62 ya nyumba zote huko Gaza," Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA) limesema katika ripoti.
Kulingana na taarifa ya UNRWA, ripoti hiyo ilitumia picha za satelaiti kutathmini uharibifu huo.
Ripoti hiyo pia iligundua kuwa vita vimeacha "asilimia 84 ya vituo vyote vya afya" huko Gaza vikiwa vimeharibiwa au kubomolewa kikamilifu na pia kuathiri sana mfumo wa elimu katika ukanda huo.
Aidha ripoti hiyo imebaini kuwa: "Watoto 625,000 huko Gaza hawako shuleni kwani mfumo wa elimu umeporomoka."
UNRWA imesema kwamba vita hivyo vimesababisha "uharibifu usio na kifani", na "matokeo mabaya ya afya ya kijamii na kiakili" kwa wanawake, vijana, na idadi ya watu walio hatarini.
Shirika hilo la UN limebainisha kuwa karibu mashirika 980 yasiyo ya kiserikali yaliyosajiliwa Gaza yamesitisha shughuli zao, na hivyo kuzidisha hali mbaya ya kibinadamu huko, huku kukiwa na wasiwasi wa kiusalama.
Kulingana na taarifa hiyo, idadi ya misaada inayoingia Gaza kwa njia ya ardhini kupitia njia ya Karem Abu Salem (Kerem Shalom) na kivuko cha Rafah "imesalia chini sana" ya lengo.
Israel ilianzisha vita vyake vya mauaji ya kimbari huko Gaza tarehe 7 Oktoba baada ya kundi la muqawama la Hamas la Palestina kutekeleza Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa dhidi ya utawala huo ghasibu ili kulipiza kisasi kwa ukatili wake dhidi ya watu wa Palestina.
Utawala wa Israel pia umeweka "mzingiro kamili" dhidi ya eneo hilo, kukata mafuta, umeme, chakula na maji kwa Wapalestina zaidi ya milioni mbili wanaoishi huko.
Tangu kuanza kwa mashambulizi hayo, utawala wa Tel Aviv umeua Wapalestina wasiopungua 33,100 na kuwajeruhi wengine karibu 75,750.