AFC yataka FIFA iifutie uanachama Israel kutokana na jinai zake Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i111832-afc_yataka_fifa_iifutie_uanachama_israel_kutokana_na_jinai_zake_gaza
Shirikisho la Soka Asia (AFC) limetangaza kuunga mkono ombi la Palestina la kulitaka Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) liifutie uanachama Israel katika taasisi hiyo kubwa zaidi ya kandanda duniani, kutokana na utawala huo wa Kizayuni kutenda jinai kubwa dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2024-05-16T12:21:08+00:00 )
May 16, 2024 12:21 UTC
  • AFC yataka FIFA iifutie uanachama Israel kutokana na jinai zake Gaza

Shirikisho la Soka Asia (AFC) limetangaza kuunga mkono ombi la Palestina la kulitaka Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) liifutie uanachama Israel katika taasisi hiyo kubwa zaidi ya kandanda duniani, kutokana na utawala huo wa Kizayuni kutenda jinai kubwa dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Katika Mkutano wa 34 wa AFC uliomalizika leo Alkhamisi katika mji mkuu wa Thailand, Bangkok, Rais wa Shirikisho la Kandanda Asia, Sheikh Salman bin Ebrahim Al Khalifa amesema wanaunga mkono muswada wa Shirikisho la Soka la Palestina PFA, wa kutaka Israel ipokonywe uanachama ndani ya FIFA.

Amesema, AFC ni madhubuti tu iwapo wanachama wake watakuwa madhubuti, na kwamba iwapo mwanachama mmoja atakumbwa na matatizo, basi matatizo hayo yataathiri wanachama wengine.

Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) linatazamiwa kupiga kura katika mkutano wake ujao mjini Bangkok kesho Ijumaa, kuhusu ombi la Shirikisho la Soka la Palestina la kuiondoa Israel katika uanachama wa FIFA.

Aidha Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mwezi Februari mwaka huu pia liliiandikia barua FIFA, likiitaka isitishe shughuli zote za soka za utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na utawala huo kutenda jinai huko Gaza.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Palestina, mamia ya wachezaji wa Kipalestina wameuawa shahidi na kujeruhiwa, pamoja na kubomolewa kwa viwanja vya soka huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, tangu kuanza kwa vita vya Gaza Oktoba 7, 2023, vilivyoua Wapalestina zaidi ya 35,000.