Maandamano ya watu milioni moja Sana'a Yemen kuunga mkono Wapalestina Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i112160-maandamano_ya_watu_milioni_moja_sana'a_yemen_kuunga_mkono_wapalestina_gaza
Mji mkuu wa Yemen, Sana'a, Ijumaa ulishuhudia maandamano ya watu milioni moja kwa ajili ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina, wakitaka kuendelea kuungwa mkono Wagaza hadi ushindi wao wa mwisho dhidi ya utawala wa Israel.
(last modified 2024-05-25T03:47:14+00:00 )
May 25, 2024 03:47 UTC
  • Maandamano ya watu milioni moja Sana'a Yemen kuunga mkono Wapalestina Gaza

Mji mkuu wa Yemen, Sana'a, Ijumaa ulishuhudia maandamano ya watu milioni moja kwa ajili ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina, wakitaka kuendelea kuungwa mkono Wagaza hadi ushindi wao wa mwisho dhidi ya utawala wa Israel.

Katika Medani ya Al-Sabeen mjini Sana'a, umati mkubwa wa watu ulipiga nara zinazounga mkono msimamo wa Yemen katika kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na kuapa kwamba hawatarudi nyuma hata wakishinikizwa kwa vitisho.

Umati huo wa watu ulinyanyua bendera na mabango ya Yemen na Palestina ukilaani mauaji na vita vya maangamizi vilivyoanzishwa na Marekani na utawala wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina kwa zaidi ya miezi saba.

Baadhi ya mabango yamelaani misimamo dhaifu ya baadhi ya nchi za Kiarabu na Kiislamu kuhusu vita dhidi ya Gaza.

Umati huo wa watu milioni moja umepongeza oparesheni zinazofanywa na jeshi la Yemen katika Bahari ya Sham, Bahari ya Arabia, Ghuba ya Aden, Bab al-Mandab na Bahari ya Mediterania kuzuia kupita katika maeneo hayo meli zinazofungamana na utawala wa Israel, Marekani na Uingereza.

Waandamanaji Yemen wamemuenzi shahidi Ebrahim Raisi kutokana na misimamo yake imara ya kutetea wanayonge na Qur'ani Tukufu

Vile vile wamesisitiza kuwa hakuna mstari mwekundu kwa jeshi la Yemen na kwamba hujuma yoyote itakabiliwa na hujuma.

Washiriki wa mjumuiko huo pia walitoa salamu za rambirambi kwa wananchi wa Iran kwa kufa shahidi Rais Ebrahim Raisi na maafisa aliokuwa ameandamana nao katika ajali ya helikopta.