UNFPA: Nusu ya watu wa Gaza wanakabiliwa na hatari ya njaa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i112232-unfpa_nusu_ya_watu_wa_gaza_wanakabiliwa_na_hatari_ya_njaa
Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) limetoa onyo kali kuhusu mgogoro wa kibinadamu unaoendelea katika Ukanda wa Gaza, likisema nusu ya wakazi wa eneo hilo wako katika hatari ya "njaa inayokaribia."
(last modified 2024-05-27T02:21:53+00:00 )
May 27, 2024 02:21 UTC
  • UNFPA: Nusu ya watu wa Gaza wanakabiliwa na hatari ya njaa

Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) limetoa onyo kali kuhusu mgogoro wa kibinadamu unaoendelea katika Ukanda wa Gaza, likisema nusu ya wakazi wa eneo hilo wako katika hatari ya "njaa inayokaribia."

Shirika hilo liliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X siku ya Jumapili kwamba: "Nusu ya watu wote Gaza wako katika hatari ya njaa inayokaribia, ikiwa ni pamoja na wanawake wajawazito 15,000."

UNFPA imethibitisha kwamba njaa huko Gaza ni jambo ambalo limesababishwa na binadamu ikiashiria vita vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya eneo hilo tangu Oktoba mwaka jana.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeendelea kusema kuwa njaa huko Gaza ni matokeo ya moja kwa moja ya Israel kufunga vivuko vya eneo hilo na kukata upatikanaji wa misaada, likisisitiza haja ya dharura ya kusitishwa mapigano mara moja huko Gaza kutokana na mahitaji makubwa ya wakazi kupata usaidizi wa kibinadamu.

Onyo la UNFPA limekuja baada ya mashirika sabini ya kutetea haki za binadamu kutoa tamko la pamoja, yakitoa wito kwa mamlaka husika na taasisi za kimataifa kutambua rasmi hatari ya janga la njaa katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa.

Kundi hilo lilijumuisha Euro-Med Human Rights Monitor, Shirika la Kimataifa la Wanasheria, Shirika la Kimataifa la Kutokomeza Aina Zote za Ubaguzi wa Rangi, Muungano wa Wanasheria wa Kiarabu na Shirika la Haki za Binadamu la Kiarabu.