Hamas: Israel inatumia mazungumzo kuendeleza mauaji ya kimbari Gaza
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, amesema kuwa, utawala ghasibu wa Israel unarefusha kwa makusudi mazungumzo ya usitishaji vita ili kuendeleza vita vyake vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina Ukanda wa Ghaza.

Ismail Haniya ameyasema hayo siku ya Ijumaa, alipohutubia kikao katika mji mkuu wa Lebanon Beirut.
Hata hivyo, aliongeza kuwa makundi ya muqawama hayakubali kuwa sehemu ya ujanja huo wa utawala haramu wa Israel
Ikumbukwe kuwa, utawala katili wa Israel ulianzisha vita dhidi ya Gaza mwezi Oktoba ili kukabiliana na operesheni ya Hamas ya Kimbunga cha Al-Aqsa iliyotekelezwa ili kulipiza kisasi jinai za miongo kadhaa za Israel dhidi ya Wapalestina.
Mashambulizi ya kijeshi ya Israel dhidi ya Gaza tokea wakati huo hadi sasa yamesababisha vifo vya Wapalestina 36,224 wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Misri na Qatar ni wapatanishi katika mazungumzo yenye lengo la kuhitimisha vita vya Gaza. Katika mapatano ya awali mwezi Novemba mwaka jana Hamas iliwaachilia mateka 105 Wazayuni ambao walikuwa wamewakamata wakati wa Operesheni ya Kimbunga cha Al Aqsa.
Mapema mwezi wa Mei, Hamas ilikubali pendekezo lingine la mapatano la kuwezesha kusitishwa kwa uvamizi wa Israel na kuachiliwa kwa wafungwa wengine. Utawala wa Israel ulionyesha ukaidi na kiburi na kukataa pendekezo hilo.
Kwingineko katika matamshi yake, Haniya alibainisha kwamba operesheni ya "Kimbunga cha Al-Aqsa iliinua kadhia ya Palestina kwa kiwango kisicho na kifani na ikafungua mlango wa kutambuliwa taifa la Palestina."
Alikuwa akiashiria mataifa matatu ya Ulaya ya Uhispania, Ireland, na Norway ambayo hivi karibuni yametangaza kutambua Palestina katika pigo kwa utawala wa Israel.