Hamas ni sehemu ya msingi ya kisiasa ya Gaza, haiwezi kupuuzwa
Mjumbe wa ngazi za juu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, amesema harakati hiyo yenye makao yake Gaza ni sehemu isiyoweza kutenganishwa katika mazingira ya kisiasa ya Gaza.
Ghazi Hamad alisema hayo katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Al Araby chenye makao yake nchini Qatar Jumatatu usiku akijibu tangazo la Rais wa Marekani Joe Biden siku ya Ijumaa kwamba Israel "imetoa ramani mpya ya awamu tatu" ili kukomesha mauaji yake ya kimbari ya takriban miezi minane dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
Pendekezo hilo la kusitisha mapigano linajumuisha mpango wa awamu tatu, kubadilishana mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina, kuondolewa kwa majeshi ya Israel kutoka Gaza na kujengwa upya eneo hilo la pwani lililoharibiwa.
Pendekezo hilo la Biden linataka Hamas iondolewe madarakani Gaza jambo ambalo kundi hilo limelipinga mara kwa mara. Hamas ilichaguliwa kidemokrasia na wapalestina wa Gaza kuongoza eneo hilo.
Hamad amesema pendekezo la usitishaji vita Gaza lililotangazwa na rais wa Marekani linatiliwa shaka.
Afisa huyo mkuu wa Hamas amesisitiza kuwa utawala ghasibu wa Israel unakusudia kupotosha pande nyingine zinazohusika katika mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza ili kuendeleza mashambulizi yake ya umwagaji damu dhidi ya eneo hilo la pwani lililozingirwa.
Hamad amedokeza kuwa: "Harakati ya Hamas haitaondoka kamwe katika mazingira ya kisiasa ya [Gaza]. Wazayuni na Wamarekani wanaota ndoto za mchana kuhusu dhana hiyo ya kipuuzi.”
Aidha amebainisha kuwa Wapalestina wataunda mustakabali wa Gaza mara tu vita vikali vinavyolikumba eneo hilo vitakapomalizika.
Tokea Oktoba 7, utawala haramu wa Israel umeua takriban Wapalestina 36,479, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na watu wengine 82,777 wamepata majeraha makali. Zaidi ya watu milioni 1.7 wamekuwa wakimbizi wa ndani wakati wa vita hivyo vya mauaji ya kimbari.