Yemen yashambulia Bandari ya Eilat kwa makombora ya balestiki
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i114316-yemen_yashambulia_bandari_ya_eilat_kwa_makombora_ya_balestiki
Vikosi vya Wanajeshi wa Yemen vimeipiga kwa makombora ya balestiki Bandari ya Eilat, kusini ya maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel, katika operesheni ya kulipiza kisasi.
(last modified 2024-07-21T07:33:17+00:00 )
Jul 21, 2024 07:33 UTC
  • Yemen yashambulia Bandari ya Eilat kwa makombora ya balestiki

Vikosi vya Wanajeshi wa Yemen vimeipiga kwa makombora ya balestiki Bandari ya Eilat, kusini ya maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel, katika operesheni ya kulipiza kisasi.

Msemaji wa vikosi hivyo, Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema hayo leo Jumapili na kueleza kuwa, vikosi vya Yemen vimefanikiwa pia kulenga meli za utawala haramu wa Israel na Marekan katika Bahari Nyekundu pamoja na Bandari ya Eilat.

Jenerali Saree ameeleza kuwa, vikosi vya Yemen vimevurumisha makombora kadhaa ya balestiki ambayo yamepiga kwa usahihi mkubwa maeneo kadhaa ya "Israel" katika Bandari ya Eilat.

Amesema vikosi vya wanamaji vya nchi hiyo vile vile vimefanya operesheni kadhaa dhidi ya meli za kibiashara za Marekani, Uingereza na utawala wa Kizayuni wa Israel katika maji ya Bahari ya Sham.

Saree ametaja meli ya Marekani iiliyolengwa kwenye operesheni hiyo kuwa ni “Pumba” na kubainisha kuwa meli hiyo imelengwa kwa makombora ya balestiki na ndege zisizo na rubani. Brigedia Jenerali saree anasisitiza kuwa, operesheni hiyo imefanikiwa kwa asilimia 100.

Hudaydah ilivyoshambuliwa na utawala wa Kizayuni

Amesema vikosi vya Yemen vimefanya mashambulio hayo, kujibu mashambulizi ya anga yaliyofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya mji wa al-Hudaydah, magharibi mwa Yemen. Watu kadhaa wameuawa na kujeruhiwa katika hujuma hizo za kinyama za Wazayuni.

Saree amesisitiza kwamba, vikosi vya jeshi la Yemen vimejiandaa kwa vita vya muda mrefu na adui Mzayuni, hadi uchokozi dhidi ya Gaza utakapokoma, mzingiro uondolewe, na uhalifu wote unaofanywa dhidi ya watu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza ukomeshwe.