Amnesty International: Marekani mshirika wa Israel katika mauaji ya kimbari Palestina
Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International imeonya Marekani kuhusu kuupa silaha utawala wa Kizayuni katika vita vya Gaza na kutangaza kuwa, Washington ni mshirika wa utawala huo katika mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.
Kwa mujibu wa mtandao wa Al Jazeera; Paul O'Brien, Mkurugenzi Mtendaji wa Amnesty International ameeleza kuwa, Marekani inafahamu kuwa Israel inatumia kinyume cha sheria silaha zilizotengenezwa na Marekani kwa uhalifu wa kivita (huko Gaza) na hii inamaanisha kuwa Washington inahusika katika uhalifu huu kutokana na kuupatia silaha utawala wa Israel.
Afisa huyu mwandamizi wa Amnesty International amebainisha kuwa, serikali ya Marekani imepokea ushahidi mwingi kutoka kwa wataalamu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kuhusu matumizi ya silaha za Washington katika jinai za kivita na mauaji ya watu kinyume cha sheria yanayofanywa na Israel.
Sambamba na kuionya Ikulu ya White House kuhusu sera zake kuhusu vita vya Gaza, mkurugenzi wa Amnesty International amesema kuwa, nchi yoyote itakayojaribu kutuma silaha kwa nchi ambayo inakiuka sheria za kimataifa haitakiuka tu wajibu wake wa kuheshimu sheria za kimataifa bali itakuwa inasaidia kutokea kwa matukio haya dhidi ya binadamu na vitendo haramu.
Marekani ambayo inadai kuwa mtetezi wa haki za binadamu imekuwa ikikosolewa na walimwengu kutokana na hatua yake ya kuendelea kuupatia silaha utawala haramu wa Israel ambao unatumia silaha hizo kufanya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.