Umoja wa Mataifa: Hali katika Ukanda wa Gaza ni maafa kikamilifu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, hali katika Ukanda wa Gaza iliyosababishwa na mashambulizi ya Israel ni maafa kamili ambayo hayajawahi kuonekana katika medani yoyote ya vita.
Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisisitiza: Tangu niwe Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, nimeshuhudia mauaji na uharibifu wa hali ya juu zaidi huko Gaza.
Guterres amefahamisha kuwa, kiwango cha misaada ya kibinadamu kwa Ukanda wa Gaza hakiendani kikamilifu na mahitaji, na kuongeza: "Tuko katika hali ya uvunjaji sheria kabisa, na hakuna anayehusika na usalama popote katika eneo la Gaza, na misafara ya misaada ya kibinadamu katika eneo hilo inavamiwa na kuporwa.
Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, asilimia 90 ya wakaazi wa Ukanda wa Gaza wameyakimbia makazi yao baada ya hujuma na uvamizi wa jeshi la Israel dhidi ya eneo hilo.
Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa, zaidi ya wafanyakazi 300 wa sekta ya afya, vikosi 35 vya ulinzi wa raia na wafanyakazi 135 wa Shirika la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) wameuawa shahidi katika hujuma inayoendelea ya utawala ghasibu wa Israel.
Uungaji mkono wa wazi wa Marekani na nchi za Magharibi umepelekea kushuhudiwa faili jeusi la viongozi watenda jinai wa utawala wa Kizayuni wanaoua watu wasio na ulinzi wala hatia. Bila shaka wale wote wanaohami na kuunga mkono jinai za Israel wanahusika pia katika jinai na mauaji ya kimbari ya utawala huo katika Ukanda wa Gaza.