Wazayuni washambulia tena shule na kuua makumi ya watu Gaza
(last modified Wed, 21 Aug 2024 02:58:24 GMT )
Aug 21, 2024 02:58 UTC
  • Wazayuni washambulia tena shule na kuua makumi ya watu Gaza

Mashambulizi ya Israel dhidi ya Shule ya Mustafa Hafez inayohifadhi wakimbizi wa Kipalestina magharibi mwa Ukanda wa Gaza yameua takriban raia 20 na kujeruhi wengine wengi.

Mashuhuda wa shambulio hilo na vyanzo vya matibabu vinasema kwamba, inatarajiwa kwamba idadi ya wahanga wa shambulio hilo la jana Jumanne la Israeli dhidi ya Shule ya Mustafa Hafez itaongezeka.

Shirika la habari la Iran Press limeandika habari hiyo na kueleza kwamba, aghalabu ya waathiriwa wa ukatili huo wa Wazayuni ni watoto wadogo. Majengo ya Shule ya Mustafa Hafez inayohifadhi Wapalestina 700 waliokimbia makazi yao yameharibiwa vibaya katika shambulio hilo la Israel.

Aidha mapema jana, raia sita waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika shambulio jingine la Israeli dhidi ya nyumba moja kwenye kambi ya wakimbizi ya Bureij katikati mwa Gaza.

Mashambulio ya kinyama ya jeshi la utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza yangali yanaendelea huku takwimu zikionyesha kuwa, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi hadi sasa ikiwa imeshapindukia 40,000.

Utawala wa Kizayuni umeendelea kukaidi kutekeleza azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka kusitishwa mara moja mapigano, huku ukiandamwa na shutuma za kimataifa kwa kuendeleza mashambulizi ya kikatili na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza tokea Oktoba 7 mwaka jana.