Maafisa wa UNRWA: Kila kitu cha maafa kinachoonekana Ghaza hakijawahi kutokea
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i115688-maafisa_wa_unrwa_kila_kitu_cha_maafa_kinachoonekana_ghaza_hakijawahi_kutokea
Maafisa waandamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina UNRWA wamesema, maafa na masaibu yanayowapata Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza hayajawahi kutokea.
(last modified 2024-08-27T03:20:14+00:00 )
Aug 27, 2024 03:20 UTC
  • Maafisa wa UNRWA: Kila kitu cha maafa kinachoonekana Ghaza hakijawahi kutokea

Maafisa waandamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina UNRWA wamesema, maafa na masaibu yanayowapata Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza hayajawahi kutokea.

Louise Wateridge, Afisa  Mwandamizi wa Mawasiliano wa UNRWA na Sam Rose, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa UNRWA katika maeneo ya nje ya ofisi, kutoka Deir Al Balah huko Ghaza, wameeleza hayo katika mkutano waliofanya na waandishi wa habari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kwa njia ya mtandao.

Wateridge amesema, "kila kitu kinachoonekana hapa, hakijawahi kutokea. Kila kitu ambacho Umoja wa Mataifa umefikia katika Ukanda wa Ghaza hakijawahi kutokea na kila siku ni changamoto mpya.”

Afisa huyo wa UNRWA amefafanua kwa kusema: "kueilezea hali ya hapa, ni janga tu. Wiki kadhaa zilizopita tumekuwa na maagizo ya kulazimishwa ya kuhama katika eneo la katikati, katika eneo la kusini, na pia kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza, na tunachokiona hapa ni mamia ya maelfu ya watu kulazimishwa kuhama kila siku.” 

Louise Wateridge (kushoto) na Sam Rose

Wateridge ameyaelezea mazingira ya madhila na mateso wanayopitia kila uchao Wapalestina wa Ghaza akisema: “watu hawajui pa kwenda. Ikiwa utaona eneo la kibinadamu, ikiwa unaona kando ya eneo hilo, ni vigumu hata kuona tena mchanga wa sakafu. Ni mrundikano wa makazi ya watu. Watu wanatumia mchanga na kujenga kuta kwa mchanga kuzuia maji ya bahari kuingia kwenye makazi yao ya muda".

Ameendelea kueleza: "kuna nge, kuna mbu, panya na nyoka. Miongoni mwa watu wanaoishi katika hali hizi, tunaona ongezeko la kuenea kwa magonjwa. Kama wengi wanavyofahamu, sasa tumekuwa na mgonjwa wa kwanza aliyethibitishwa wa polio katika Ukanda wa Ghaza tangu miaka 25 iliyopita, na hii inabainisha tu jinsi hali ilivyo mbaya hapa".

Kwa upande wa Sam Rose yeye amesisitiza kwa kusema: "eneo la kibinadamu lililotangazwa na Israel limepungua. Sasa ni takribani asilimia 11 ya Ukanda wote wa Ghaza, na hii si asilimia 11 ya ardhi ambayo inafaa kwa makazi, wala kufaa kwa huduma, wala kwa ajili ya kuishi".../