Kifo cha Mmarekani Mturuki kimedhihirisha unafiki na undumilakuwili wa Marekani
Sep 07, 2024 11:05 UTC
Msimamo wa Marekani wa kutoa mijibizo tofauti kuhusiana na vifo vya raia wake waliouliwa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel na wale waliofariki katika matukio mengine umedhihirisha unafiki na undumilakuwili wa serikali ya Washington.
Hayo yameelezwa na Sultan Barakat, Profesa wa Taaluma ya Sera za Umma katika Chuo Kikuu cha Hamad Bin Khalifa cha Qatar katika mahojiano na televisheni ya Al Jazeera akisisitiza kwamba majibu tofauti yaliyotolewa na serikali ya Marekani kwa mauaji ya raia wake yanatoa mguso na yanatafakarisha.
Barakat amesema, serikali ya Washington imeyataja mauaji ya mwanaharakati Mmarekani mwenye asili ya Uturuki Aysenur Ezgi Eygi kuwa ni tukio la kusikitisha na kutosheka na kutoa mwito tu kwa muitifaki wake wa karibu Israel wa kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo.
Hata hivyo kwa mujibu wa msomi huyo, Marekani, na kinyume chake, imeonyesha msimamo mkali kuhusiana na kifo cha mateka Muisraeli Marekani Hersh Goldberg-Polin kilichotokea huko Ghaza ambapo mbali na kulaani vikali, rais wa nchi hiyo Rais Joe Biden, alisema, "viongozi wa Hamas watalipa gharama ya uhalifu huu."
Biden alitoa kauli hiyo ya vitisho dhidi ya viongozi wa Hamas wakati harakati hiyo ya Palestina imeeleza bayana kuwa mateka huyo na wenzake watano waliuawa kutokana na shambulio la jeshi la Israel dhidi ya Ghaza.
Kabla ya hapo mashambulio ya jeshi la Kizayuni dhidi ya Ghaza yalishaua mateka kadhaa Waisraeli wakiwemo mateka wawili waliokuwa wamebeba bendera nyeupe ya kujisalimisha kwa askari wa jeshi hilo.
Itakumbukwa kuwa mnamo Mei 11, 2022 pia askari wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel walimuua kwa kumpiga risasi mwandishi wa habari Mpalestina Mmarekani Shireen Abu Akleh, alipokuwa akiiripotia televisheni ya Aljazeera katika kambi ya Wapalestina ya Jenin, Ukingo wa Magharibi.
Kufuatia mauaji hayo, serikali ya Marekani sio tu haikuchukua hatua wala kutoa kauli yoyote kali dhidi ya Israel, lakini ilitosheka na kutoa taarifa tu iliyoeleza kwamba mauaji hayo hayakufanywa kwa makusudi.../