Maandamano makubwa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ya kupinga vita
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i116224-maandamano_makubwa_katika_ardhi_zinazokaliwa_kwa_mabavu_ya_kupinga_vita
Vyombo vya habari vya Israel vimetangaza kuwa, takriban watu nusu milioni katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu (Israel) wametoa wito wa kusitishwa kwa vita vya Gaza kwa kufanya maandamano dhidi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na baraza lake la mawaziri.
(last modified 2024-09-10T22:50:09+00:00 )
Sep 10, 2024 22:50 UTC
  • Maandamano makubwa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ya kupinga vita

Vyombo vya habari vya Israel vimetangaza kuwa, takriban watu nusu milioni katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu (Israel) wametoa wito wa kusitishwa kwa vita vya Gaza kwa kufanya maandamano dhidi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na baraza lake la mawaziri.

Mwezi wa 11 wa vita dhidi ya Gaza pia umemalizika na vita hivi sasa vinakaribia kutimiza mwaka mmoja tangu vilipoanza. Tukio muhimu zaidi wakati huu wa kukaribia mwaka mmoja wa vita ni kuanza duru mpya ya maandamano makubwa dhidi ya Netanyahu na baraza lake la mawaziri. Vyanzo vya habari vya utawala wa Kizayuni vilitangaza Jumamosi usiku kuwa maandamano makubwa zaidi yalifanyika Tel Aviv tangu kuanza kwa vita dhidi ya Gaza tarehe 7 Oktoba 2023.

Kanali ya habari ya Kizayuni ya Kan imetangaza kuwa, idadi ya waandamanaji mjini Tel Aviv ilikuwa zaidi ya watu nusu milioni. Waandaaji wa maandamano hayo pia wamekadiria idadi ya waandamanaji kuwa karibu watu nusu milioni.

Swali muhimu ni kwa nini maandamano makubwa na ambayo hayajawahi kutokea yamefanyika wakati huu wa vita? Katika kujibu swali hili, inapasa kuashiria miili sita ya matekka wa Kizayuni iliyopatikana huko kusini mwa Gaza. Duru mpya ya maandamano makubwa dhidi ya Benjamin Netanyahu ilianza wakati miili ya mateka sita ilipopatikana kusini mwa Gaza. Waandamanaji wanamtuhumu Benjamin Netanyahu kwa kuwatoa muhanga mateka wa Kizayuni ili yeye abakie madarakani na hana nia ya kumaliza mkwamo katika mazungumzo ya kusitisha vita na kubadilishana mateka.

Jambo muhimu kuhusu maandamano haya ni kwamba, hayakuishia Tel Aviv pekee, bali yalifanyika pia katika miji mingine ya maeneo yaliyotwaliwa kwa kuhudhuriwa na matabaka mbalimbali za jamii. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana  wataalamu wa masuala ya kisiasa wa utawala wa Kizayuni wameyataja maandamano hayo katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kuwa ya kihistoria na yasiyo na kifani.

 

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, maandamano hayo hayawezi kuupuuzwa kwa sababu si kama maandamano ya mwezi mmoja au miwili iliyopita, bali ni maandamano ya kweli na yenye ujumbe mzito ambapo makundi mbalimbali ya jamii ya Kizayuni yalishiriki ili kumshinikiza Netanyahu kutia saini makubaliano ya kubadilishana mateka.

Nukta nyingine muhimu ni kwamba, maandamano hayo makubwa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina bandia la Israel yameonyesha kuwa, kuna pengo kubwa kati ya matakwa ya wananchi na utendaji wa baraza la mawaziri la Netanyahu kuhusiana na vita vya Gaza. Wakati watu wakifanya maandamano ambayo hayajawahi kushuhudiwa kuunga mkono kutiwa saini makubaliano ya kubadilishana mateka na muqawama, baraza la mawaziri la Netanyahu linasisitiza juu ya kuendelea kwa vita.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahuu

 

Pengo hili limekuwepo kati ya wananchi na baraza la mawaziri huko nyuma, lakini halikuonekana hadharani na kwa sura kubwa namna hii. Kwa mantiki hiyo basi vyombo vya habari vya Kizayuni vimeripoti kuwa, waandamanaji wa Tel Aviv na miji mingine ya Israel waliingia mitaani na kutaka Netanyahu aondolewe madarakani.

Nukta ya mwisho ni kwamba, familia za mateka hao wa Kizayuni zimetaka kuweko uingiliaji kati wa Marekani na mashinikizo ya Washington dhidi ya Netanyahu kwa ajili ya kuhitimisha vita hivyo na kufikia natija mazungumzo ya usitishaji vita. Familia hizi zilisisitiza kwa kutoa taarifa: Hamas ilikubali makubaliano ya kubadilishana mateka mwezi Julai, lakini Netanyahu alichezea shere mazungumzo; kwa hiyo, serikali ya Marekani haipaswi kuruhusu Netanyahu aendelee na vitendo hivi.