Sep 13, 2024 11:44 UTC
  • WHO: Wapalestina 22,000 wanateseka na majeraha yanayobadili maisha

Ripoti mpya ya Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO imebaini kwamba kwamba takriban robo ya Wapalestina waliojeruhiwa katika vita vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya Gaza ambao ni sawa na watu 22,500 wanakabiliwa na majeraha ya kubadilisha maisha ambayo yanahitaji huduma za marekebisho  sasa na kwa miaka ijayo.

Dkt. Richard Peppercorn, Mwakilishi wa WHO katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Palestina, amesema ongezeko kubwa la mahitaji ya urekebishaji wa viungo linatokea sambamba na "uharibifu unaoendelea wa mfumo wa hudumuma za afya".

Amesisitiza kuwa maisha ya wagonjwa yako hatarini kwani huduma za urekebishaji viungo wa papo hapo zimetatizika sana na huduma maalum kwa majeraha makubwa yenye utata haipatikani.

WHO inasema hivi sasa, ni hospitali 17 tu kati ya 36 za Gaza ambazo zimesalia zikifanya kazi kwa kiasi, wakati huduma za afya ya msingi na huduma za ngazi ya jamii zinasitishwa mara kwa mara au hazipatikani kwa urahisi kutokana na mashambulizi yanayotekelezwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Hadi sasa Wapalestina wapatao 41,084 wameuawa shahidi na 95,029 wamejeruhiwa katika vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza. Aghalabu ya Wapalestina waliouawa shahidi ni wanawake na watoto.