Sheikh Naim Qassim: Tumejiandaa kikamilifu kukabiliana na Israel
(last modified Mon, 30 Sep 2024 14:10:45 GMT )
Sep 30, 2024 14:10 UTC
  • Sheikh Naim Qassim: Tumejiandaa kikamilifu kukabiliana na Israel

Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema, harakati hiyo imejiandaa kikamilifu kukabiliana na mashhambulio ya utawala haramu wa Israel.

Sheikh Naim Qassim, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema hayo kwa mnasaba wa kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah na makamanda kadhaa wa Hizbullah na kueleza kwamba,"Katu hatutalegeza misimamo yetu hata kidogo na tutaendelea kuiunga mkono Gaza katika fremu ya ulinzi wa Palestina."

Aidha amesema, Israel inashambulia ardhi na raia wa Lebanon na kufanya jinai na mauaji makubwa kwa uungaji mkono kamili wa Marekani.

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah amebainisha kwamba, ikiwa Israel itaamua kuingia Lebanon kwa njia ya nchi kavu, vikosi vya muqawama viko tayari kukabiliana na mashambulio ya ardhini.

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema: Uwezo wetu ni mkubwa na adui ameingia kichaa kutokana na kushindwa kufikia mamlaka yetu.

Shahidi Sayyid Nasrullah

 

Aidha Sheikh Naim Qassim amesisitiza: Tuna imani kwamba adui hatafikia lengo lake na tutatoka ndani ya uwanja huu tukiwa washindi.

Katika upande mwingine, Sheikh Naim Qassim ameongeza kuwa: Shahidi Seyyed Hassan Nasrullah kipaumbele chake daima kilikuwa Quds Tukufu katika fremu ya umoja wa Kiarabu na Kiislamu.

Kiongozi huyo mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa, harakati hiyo imejiandaa kikamilifu kukabiliana na adui Mzayuni na kwamba, kuuawa shahidi Nasrullah hakutatia dosari katika azma na irada ya wanamuqawama shupavu wa Lebanon.