Israel inazuia kuenezwa ripoti kuhusu pigo kubwa ililopata kufuatia shambulizi la Iran
Utawala haramu wa Israel umefunga vituo kadhaa muhimu vya kijeshi na kuzuia uchapishaji wa ripoti kuhusu athari za mashambulio ya hivi karibuni ya makombora ya Iran dhidi ya utawala huo ghasibu.
Tovuti ya habari ya Middle East Eye iliripoti Jumatano kwamba Israel inabana habari kikamilifu na hivyo ni vigumu kutathmini uharibifu kamili uliosababishwa na shambulio la kulipiza kisasi la Iran siku ya Jumanne.
Utawala wa Israel umedai kuwa makombora mengi yalinaswa, lakini kanda za video mtandaoni zilionyesha makombora mengi yakitua na kuripuka ndani ya ngome za kijeshi na kijasusi za utawala huo ghasibu.
Operesheni ya Iran, iliyopewa jina la Operesheni ya Ahadi ya Kweli II, ilitekelezwa kujibu vitendo vya kinyama vya Israel vya mauaji dhidi ya viongozi wakuu wa upinzani.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Jumanne usiku lilitoa taarifa likitangaza kuwa limeshambulia kitovu cha maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina (Israel) ikiwa ni katika kujibu mauaji ya shahidi Ismail Haniya, Sayyid Hassan Nasrullah na Meja Jenerali Abbas Nilforoushan, Kamanda na mshauri wa ngazi ya juu wa IRGC huko Lebanon. Oparesheni hiyo kwa jina la Ahadi ya Kweli ya Pili imetekelezwa kwa idhini ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na baada ya kujulishwa kamandi kuu ya vikosi vya ulinzi na kuungwa mkono na jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Wizara ya Ulinzi.