Kusalia Imara Mhimili wa Muqawama
(last modified Fri, 11 Oct 2024 02:35:29 GMT )
Oct 11, 2024 02:35 UTC
  • Kusalia Imara Mhimili wa Muqawama

Baada ya kutekelezwa Oparesheni ya Kimbunga cha al Aqsa, Utawala wa Kizayuni wa Israel ulidhani kuwa ungeweza kuiangamiza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) kwa mashambulizi ma kubwa na kuigeuza Gaza kuwa ardhi iliyoungua.

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita wanawake, watoto na vijana wa Kipalestina zaidi ya elfu 50 wameuawa shahidi, makumi ya maelfu wamejeruhiwa na Wapalestina milioni mbili wamekuwa wakimbizi. Sehemu kubwa ya Ukanda wa Gaza pia imebomolewa na kuharibiwa. Hata hivyo harakati ya muqawama imeendelea kuwa hai na imara zaidi licha ya uharibifu wote huo na kuuawa kwa umati maelfu ya raia wa Palestina. Netanyahu, chinja chinja wa Gaza alitangaza masuala kadhaa kama vile kukomboa mateka wa Israel, kuangamizwa harakati za Hamas na Jihad Islami, kupokonywa silaha makundi ya mapambano ya Palestina, kufukuzwa katika ardhi zao raia wa Kipalestina, kutengwa eneo salama na hata kujengwa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza kuwa ndio lengo la hujuma ya Israel Ukanda wa Gaza, lakini licha ya kupita mwaka mmoja sasa tangu baada ya Oparesheni Kimbunga cha al Aqsa dhidi ya utawala huo hakuna hata lengo moja kati ya hayo lililofanikiwa. 

Hugh Lovatt, mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Baraza la Uhusiano wa Kigeni la Umoja wa Ulaya ameiambaia televisheni ya Euronews kuwa: "Inasemekana kuwa Hamas imepoteza wapiganaji 6,000, hata hivyo kidhahiri kundi hilo limeajiri na kukusanya idadi ya wanajeshi sawa kabisa na hiyo iliyotajwa, na kundi hilo limejikita pakubwa katika mustakbali wa Gaza na linataka kuendelea kusimamia masuala ya ukanda huo."  

Hugh Lovatt ameashiria baadhi ya ripoti kuhusu uwezekano wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kusimamiwa Ukanda wa Gaza na kusema kwamba: "Hebu tuweke wazi kuhusu hili. Ingawa Hamas imeathirika katika vita hivi, lakini kundi hilo haliendi popote."

Hamas bado iko hai

Naye Mustafa Barghuthi mwanasiasa mkongwe wa Kipalestina amesema katika mahojiano kuwa: "Matumaini yanazidi kuongeza miongoni kwa kizazi kipya cha Wapalestina, na kizazi hiki abadan hakitasalimu amri licha ya utawala wa Kizayuni kuendeleza jinai zake katika Ukanda wa Gaza na kubomoa shule na vyuo vikuu kwa lengo la kuangamiza kizazi cha wasomi wa Kipalestina." 

Mbali na kuvitaja vita vya sasa katika Ukanda wa Gaza kuwa ni vya uharibifu zaidi kuliko matukio yaliyojiri mwaka 1948, mwanasiasa huyo wa Palestina amesema: "Sidhani kama katika historia nzima ya sasa kuna mfano wa ukubwa wa jinai na ukatili unaofanywa na jeshi la Israel katika mashambulizi yake dhidi ya Wapalestina." Huenda Wazayuni wameweza kutoa vipigo kwa muqawama huko Palestina lakini ukilinganisha na walichopoteza mbele ya wanamapambano wa Palestina; mafanikio hayo hayasaidii lolote katika kuendeleza uwepo wa utawala bandia wa Israel. 

Katika video ya kumbukumbu ya kutimia mwaka mmoja tangu baada ya tukio la Oktoba 7 mwaka jana, Stephen Walt, profesa mtajika wa Chuo Kikuu cha Harvard amezungumzia hali ya sasa ya utawala wa Kizayuni na eneo la Mashariki ya Kati na kiwango cha mafanikio ya Marekani na utawala wa Israel katika kubadilisha taswira ya Mashariki ya Kati na kusema: "Israel imepata mafanikio ya kimbinu tu ya muda mfupi. Nina shaka kuwa matukio haya yatasababisha mabadiliko katika Mashariki ya Kati. Hamas haijashindwa huko Gaza bali imeathirika pakubwa, lakini bado ingalipo." Mhadhiri huyo mtajika wa Chuo Kikuu cha Harvard ameongeza kuwa: Mafanikio ya muda mfupi ya Israel hayatawasaidia lolote kwa muda mrefu.

Katika muktadha huo, Khaled Mash'al, mmoja wa viongozi wa Hamas anasema, licha ya hasara kubwa iliyosababishwa na vita vya mwaka mmoja huko Gaza, harakati ya muqawama ya Palestina itaibuka tena kutoka kwenye majivu kama ndege wa finikisi (phoenix). Mash'al ameongeza kuwa, Hamas inaendelea kuajiri wapiganaji na kuzalisha silaha.

Mash'al: Hamas itaibuka tena kutoka kwenye majivu kama finikisi

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika Taasisi ya Kimataifa ya Migogoro ameiambia Reuters akizungumzia maoni ya Mash'al kwamba: "Kwa ujumla, naweza kusema kuwa Hamas bado iko hai na amilifu ...."

Mojawapo ya matokeo ya mwaka mmoja wa mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina na sasa mauaji ya kikatili ya watu wa Lebanon ni kwamba kadhia ya Muqawama na mapambano dhidi ya utawala huo ghasibu imekuwa suala la kimataifa. Hadi kabla ya Oktoba 7, 2023, upinzani na ukosoaji wa aina yoyote dhidi ya jinai za Wazayuni huko Marekani na Ulaya vilitambuliwa kuwa ni chuki dhidi ya Uyahudi. Mkabala wake, uungaji mkono wowote kwa watu wanaodhulumiwa wa Palestina ulitafsiriwa katika vyombo vya habari vya Magharibi kuwa ni kuunga mkono ugaidi. Kubebwa na kunyanyuliwa juu picha za Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah, katika mitaa ya miji ya Ulaya na Marekani baada ya kuuawa, kunaonyesha vyema suala hili.

Leo hii, kufanya maandamano dhidi ya jinai za Wazayuni na kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina katika mitaa na mitandao ya kijamii na katika vyombo vingi vya habari vya nchi za Magharibi, vimekuwa nembo ya dhamiri iliyoamka ya mwanadamu.

Tags