Kushindwa mara mbili Israeli katika vita vya Lebanon
(last modified 2024-10-18T11:56:43+00:00 )
Oct 18, 2024 11:56 UTC
  • Kushindwa mara mbili Israeli katika vita vya Lebanon

Juhudi za jeshi la utawala wa Kizayuni za kujaribu kuingia katika ardhi ya Lebanon zimeshindwa na kuusababishia hasara na maafa makubwa, na kwa upande mwingine mashambulizi yake katika makazi ya raia na vituo vya vikosi vya UNIFIL nchini Lebanon yameongeza wigo wa jinai zake na hivyo kuibua hitilafu na migawanyiko kati ya waungaji mkono wake wa Magharibi.

Saa chache tu baada ya Najib Mikati, Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Lebanon, kusema kwamba alikuwa amepata dhamana kutoka kwa Marekani kwamba utawala ghasibu wa Israel utapunguza mashambulio yake katika vitongoji vya kusini mwa Beirut, mji mkuu wa nchi hiyo, jeshi la utawala huo katili lilishambulia vikali kwa mabomu makazi ya raia katika vitongoji hivyo. Isitoshe, lilishambulia pia kwa mabomu kijiji cha Muhajbib kilichoko kusini mwa Lebanon. Katika kijiji hicho cha kihistoria, lipo hekalu kongwe la Benjamini, mtoto wa Nabii Yaqub (as) lenye umri wa miaka 2100, na hili linathibitisha wazi kuwa utawala huu hauthamini hata kidogo matukufu ya Mayahudi.

Wakati huo huo, kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa chenye makao yake kusini mwa Lebanon (UNIFIL) kimetangaza kuwa kifaru cha Merkava cha utawala wa Kizayuni kilifyatua risasi kwenye mnara wa uchunguzi wa usalama wa kikosi hicho.

Wakati huo huo Wizara ya Afya ya Lebanon imetangaza kuwa, jumla ya mashahidi nchini Lebanon kutokana na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni tangu Oktoba 2023 imefikia 2,367 na idadi ya waliojeruhiwa imefikia 11,088.

Msemaji wa UNICEF katika eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini ameeleza kuwa watoto milioni 1.2 na wavulana na wasichana wadogo nchini Lebanon wanahitaji kupata elimu bora mara moja na kutangaza kuwa mwanzo wa mwaka wa shule katika shule za umma nchini Lebanon umeahirishwa na kwamba kwa sasa takriban asilimia 60 ya shule, zinatumika kama makazi ya wakimbizi.

Askari wa Kizayuni waliouawa na kujeruhiwa katika mashambulizi ya Hizbulla

Hivi sasa, Walebanon milioni moja na nusu wameacha makazi yao na kukimbilia usalama wao katika nchi jirani na za karibu kama Syria na Iraq. Ingawa moja ya malengo ya utawala wa Kizayuni katika kumuua kigaidi Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Hizbullah lilikuwa ni kuanzisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Lebanon, lakini Wakristo wa Masunni wa nchi hiyo wamewaunga mkono na kuwapa makazi ya muda wakimbizi wa Kishia na hivyo kuzima fitina za utawala wa Kizayuni kuhusu suala hilo.

Wakati huo huo Hizbullah ya Lebanon inaendeleza mapambano makali na jeshi la utawala wa Kizayuni ambalo linajaribu kupenya na kuingia katika ardhi ya Lebanon, kwa mashambulio yake ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya miji na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vilivyoko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Kulikuwa na zaidi ya kambi za kijeshi 50 za jeshi la utawala wa Kizayuni ndani ya kilomita mia moja kutoka mpaka wa Lebanon ambapo Hizbullah imelenga na kuharibu kambi zote hizo kupitia operesheni 3,000. Vituo hivyo vimeharibiwa kiasi kwamba jeshi la Israeli haliwezi tena kupeleka askari wake huko.

Hatua ya hivi karibuni ya Hizbullah ya kuipiga brigedi ya Golani ya utawala wa Kizayuni na pia kuulenga mji wa Haifa inaonesha kuwa Hizbullah ina nguvu kubwa ya kuzuia hujuma ya Wazayuni. Ijapokuwa utawala huo umetekeleza operesheni za kigaidi na kuweza kuwaua kigaidi shakhsia na viongozi muhimu wa Hizbullah lakini haujaweza kusajili mafanikio yoyote katika medani ya vita ambapo hata umeshindwa kupenya na kuingia katika maeneo yanayodhibitiwa na Hizbullah.

Kwa hakika, kimbinu Israel imepata mafanikio makubwa, lakini stratijia ya Hizbullah ya kuwatimua Wazayuni na kuifanya miji yao isiweze kukalika kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu imeifanya Hizbullah ifanikiwe zaidi, jambo ambalo limelikasirisha jeshi la Kizayuni na hivyo kulifanya lizidishe mashambulio yake ya kigaidi na kijinai dhidi ya makazi ya raia, watu na miundombinu ya Lebanon.

Shambulio la Hizbullah katika maeneo ya Wazayuni

Ushindi huu wa kimkakati unatokana na muundo madhubuti, silaha bora na za kisasa, na uelewa wa kina kuhusu muundo wa utawala haramu wa Israeli na sekta zake za kijamii, kisiasa na kijeshi. Kwa maneno mengine ni kwamba Hizbullah haifungamani na mtu binafsi na mtu mmoja anapoondoka kwa sababu moja au nyingine, nafasi yake huzibwa na mwanachama mwingine ambaye ana uwezo na nguvu zaidi.

Hizbullah ina ufahamu wa kina kuhusu Israel, nguvu, muundo wake wa kisiasa na kijamii, migawanyiko ya kijamii, pamoja na mitazamo ya watawala na walowezi wa kawaida wa utawala huo.

Uelewa huo bila shaka umeifanya Hizbullah kuwa asasi isiyo na mfano wake kati ya makundi ya muqawama na vyama vingine vya kawaida duniani.