Kuuawa shahidi Yahya Sinwar; kufedheheka Wazayuni na kubakia hai jina la Sinwar
(last modified 2024-10-19T10:57:44+00:00 )
Oct 19, 2024 10:57 UTC
  • Kuuawa shahidi Yahya Sinwar; kufedheheka Wazayuni na kubakia hai jina la Sinwar

Yayha Sinwar, Kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ameuawa shahidi na Wazayuni katika hali ambayo amepigana vita dhidi ya utawala huo hadi dakika ya mwisho ya uhai wake na hivyo kubakisha jina lake katika mioyo ya Wapalestina.

Utawala wa Kizayuni umemuua shahidi Yayha Sinwar Kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) katika jinai yake nyingine dhidi ya Gaza. Yahya Sinwar aliteuliwa kuwa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas baada ya kuuliwa shahidi Ismail Haniyeh. 

Sinwar alitumia umri wake wote wa miaka 62 kuendesha mapambano dhidi ya utawala unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu. Sinwar alifungwa miaka 23 katika jela za utawala wa Kizayuni. Utawala wa Kizayuni ulibomoa nyumba yake katika vita vya mwaka 2012, na mnamo mwaka 2015 pia Yahya Sinwar akawekwa katika orodha nyeusi ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani. Sinwar kwa muda mrefu aliwekwa katika orodha ya watu wanaosakwa na Israel; na ari ya Israel ya kutaka kumuua iliongeza hivi karibuni baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas. Vyombo vya usalama vya Israel vinaamini kuwa Sinwar alihusika katika kuratibu na kutekeleza mashambulio ya Oktoba 7 mwaka jana. Baada ya oparesheni ya "Kimbunga cha al Aqsa", jina la Sinwar lilitajwa mara kwa mara na maafisa waandamizi wa utawala wa Israel akiwemo Waziri wa Ulinzi wa utawala huo Yoav Galant. 

Shahidi Yahya Sinwar

Utawala wa Kizayuni ulijaribu kumvunjia heshima Sinwar kwa kumzulia uwongo chungu nzima kama vile eti alikuwa amejificha kwenye mahandaki na kuwatoa mhanga wakazi wa Gaza, na kwamba alikuwa amewateka nyara raia wa utawala wa Kizayuni au kwamba alikuwa amekimbilia nchini Misri. Kosa la kistratejia la Wazayuni la kurusha picha na video zinazooyesha namna Sinwar alivyouliwa shahidi limeibua kashfa kwa Wazayuni na kupelekea jina la Sinwar kusalia hai katika historia. 

Picha za kuuawa shahidi Yahya Sinwar, kiongozi wa harakati ya Hamas, ambaye alikuwa katika medani ya vita akiwa amevalia sare za mapambano na kukabiliana na utawala wa Kizayuni hadi dakika ya mwisho ya maisha yake, zimeonyesha kuwa alikuwa shujaa wa mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni. Mwandishi habari wa nchini Marekani amechapisha filamu kuhusu dakika za mwisho za harakati za mapambano ya Yahya Sinwar na kuandika: "Israel imefanya kosa kuonyesha video ya dakika za mwisho za uhai wa Sinwar. Huku akiwa amejeruhiwa vibaya akiwa amevalia skafu yake aliirushia fimbo droni iliyokuwa ikipiga picha; kitendo ambacho ni hatua ya mwisho ya kudhihirisha mapambano yake makali dhidi ya utawala wa Kizayuni. Kuuawa Sinwar kumemwachia heshima kubwa duniani na kulifanya jina lake kusalia hai daima.  

Katika hali ambayo Wazayuni wamefurahia kuuliwa shahidi Yahya Sinwar na kudai kuwa Hamas tayari imeangamizwa lakini historia inathibitisha kuwa si Hamas wala kundi lolote miongoni mwa makundi ya muqawama ambayo yatasambaratika kwa kuuliwa shahidi viongozi wake bali makundi hayo yatazidi kuimarika na kuendesha mapambano dhidi ya maghasibu wa Kizayuni. Kuhusiana na hilo, Mustafa Barghouthi, Katibu Mkuu wa Harakati ya Ubunifu wa Kitaifa ya Palestina ameashiria ushujaa wa Yahya Sinwar na kusisitiza kuwa imebainika wazi kuwa hakuwa akijificha katika njia za chini ya ardhi bali ni Netanyahu ndiye alikuwa anajificha katika njia hizo. Hata katika dakika za mwisho za maisha yake, Yahya Sinwar ameiaibisha Israeli na Netanyahu. Katibu Mkuu wa Harakati ya Ubunifu wa Kitaifa ya Palestina ameongeza kwa kuhoji: "Je, kuuawa shahidi Ahmad Yassin, Rantisi, Haniyeh na Nasrullah kumesitisha muqawama eti isemwe kwamba mapambano yamesitishwa kufuatia kuuawa shahidi al Sinwar?" Tatizo la Waisraili ni kuwa hawana ufahamu wowote kuhusu kufa shahidi na wala hawajui kuwa matarajio ya mwisho ya kila kamanda ni kufa shahidi.  

Mustafa Barghouthi 

Bassem Naim, mmoja wa maafisa wa ngazi ya juu wa harakati ya Hamas, pia ameeleza kuwa ni uchungu sana kuwapoteza wapendwa wao, hasa shakhsia kama Yahya al-Sinwar, lakini wana uhakika kwamba hatimaye wataibuka na ushindi."