Ndege ya kivita isiyo na rubani ya Hizbullah yalenga makazi ya Netanyahu + Video
(last modified 2024-10-19T11:37:43+00:00 )
Oct 19, 2024 11:37 UTC
  • Ndege ya kivita isiyo na rubani ya Hizbullah yalenga makazi ya Netanyahu + Video

Ndege ya kivita isiyo na rubani ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon imelenga makazi ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu huko Caesarea, kaskazini mwa Tel Aviv, baada ya kikosi cha anga za utawala huo kushindwa kuitungua.

Tovuti ya gazeti la Times of Israel imesema leo Jumamosi kwamba moja ya ndege zisizo na rubani tatu zilizorushwa dhidi ya Israel kutoka Lebanon mapema asubuhi ya leo zililenga "makazi ya kibinafsi ya Netanyahu katika mji wa pwani wa Caesarea, kusini mwa Haifa."

Machapisho kwenye mitandao ya kijamii ya Israel pia yamesema jengo lililopigwa katika shambulio hilo lilikuwa "sehemu ya nyumba ya Netanyahu."

Vyombo vya habari vya Israel vimekataa kutoa maelezo zaidi juu ya kiwango cha uharibifu na uwezekano wa majeruhi kufuatia kupigwa marufuku kusambazwa habari hizo na jeshi.

Ripoti zinasema Hizbullah ililenga nyumba ya kibinafsi ya Benjamin Netanyahu huko Caesarea na kwamba Netanyahu hakuwepo wakati wa shambulizi hilo.

Aidha taarifa zinasema vikosi vya utawala ghasibu wa Israel vimekiri kwamba kikosi cha ulinzi wa anga cha utawala huo ghasibu hakikuweza kuizuia ndege hiyo ya kivita isiyo na rubani ilipokuwa ikipenya katika anga ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ambayo imepachikwa jina bandia la Israel.

Klipu (hapo juu) ya ndege hiyo isiyo na rubani ya Hizbullah ikipita kando ya helikopta ya jeshi la Israel bila kutambuliwa imesambaa katika mitandao ya kijamii.

Kituo cha habari cha Lebanon cha al-Mayadeen kimelinukuu jeshi la Israel likisema kuwa ndege tatu zisizo na rubani ziliingia kutoka Lebanon hadi Haifa, huku ni mbili pekee zilizogunduliwa na kunaswa.

Vyombo vya habari vya utawala wa Israel vimezuiwa kufichua habari zaidi kuhusu shambulio hilo la Hizbullah dhidi ya makao ya Netanyahu.