Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kufuatia kuuawa shahidi Yahya al Sinwar
(last modified 2024-10-20T02:45:28+00:00 )
Oct 20, 2024 02:45 UTC
  • Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kufuatia kuuawa shahidi Yahya al Sinwar

Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ujumbe kufuatia kuuawa shahidi Yahya al Sinwar, Kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) na kusisitiza kuwa alikuwa taswira inayong'aa ya mapambano na muqawama.

Amesema: "Alisimama imara dhidi ya adui katili na mchokozi. Alimpiga adui kofi kwa tadbiri na ujasiri na kubakisha katika kumbukumbu ya historia ya eneo hili kipigo kisichoweza kufidiwa cha Oktoba 7; na kisha akajiunga na mashahidi wenzake kwa heshima na fakhari kubwa."

Shahidi Yahya Sinwar 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza kuwa: "Mtu kama Sinwar, ambaye amesabilia maisha yake katika kuendesha mapambano dhidi ya adui mvamizi na dhalimu, hana mwisho mwingine ghairi ya kufa shahidi kunakostahiki. Bila shaka kumpoteza shakhsia huyo ni jambo lenye kuhuzunisha sana na kutia uchungu kwa harakati ya muqawama, lakini harakati hiyo haikusita kusonga mbele kwa kuuawa shahidi watu watajika kama Sheikh Ahmad Yassin, Fathi Shaqaqi, Rantisi na Ismail Haniyeh; na muqawama hautasita hata kidogo kwa kuuawa shahidi Sinwar. Hamas iko hai na itaendelea kubaki hai. Kama kawaida tutaendelea kuwa bega kwa bega na pamoja na mujahidina na wanamapambano wenye ikhlasi."

Utawala wa Kizyauni umemuua shahidi Yahya Sinwar Kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) katika jinai yake nyingine dhidi ya Gaza. Yahya Sinwar aliteuliwa kuwa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas baada ya kuuawa shahidi Ismail Haniyehmjini Tehran. 

Shahidi Ismail Haniyeh 

Ayatullah Khamenei katika ujumbe wake huu kuhusu kuuawa shahidi Yahya Sinwar ameashiria nukta na masuala muhimu kuhusu nafasi ya muqawama na viongozi wa makundi hayo. Makundi ya muqawama ya Palestina yameendelea kuwa ngangari na kusimama imara dhidi ya Wazayuni baada ya kuanza oparesheni ya Kimbunga cha al Aqsa  Oktoba 7 mwaka jana licha ya mashambulizi makubwa ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza na kutoa vipigo visivyoweza kufidiwa kwa Wazayuni.  

Kinyume na madai na uwongo ya utawala wa Kizayuni, ni makundi ya mapambano ambayo yameibuka na ushindi mkubwa katika vita vya Gaza katika miezi ya karibuni; ndio maana Wazayuni wamelazimika kukiri udhaifu na kushindwa kwao mbele ya muqawama.

Jeshi la utawala wa Kizayuni limeshindwa kufanikisha malengo na kutekeleza mipango yake miovu licha ya Tel Aviv kuungwa mkono na kusaidwa kwa pande zote kisilaha na kifedha na Marekani na serikali za Magharibi; na matokeo ya kuendelea vita na mauaji ya kimbari ya utawala huo hayajakuwa na matokeo mengine isipokuwa kuzidisha hasara na maafa kwa Wazayuni mkabala wa oparesheni za makundi ya muqawama.  

Wanamuqawama wa Palestina 

Matukio ya leo katika eneo na vita vya Gaza yanaonyesha msimamo halisi wa Hamas na makundi ya muqawama ambayo yana nafasi muhimu katika kuukabili utawala wa Kizayuni na hata uungaji mkono wa Marekani haujaweza kubadili hali mbaya ya mgogoro inayousibu utawala  ghasibu wa Kizayuni.

Kiongozi Muadhamu ameashiria katika ujumbe wake suala hili muhimu na nyeti kwamba msimamo na mchango wa Sinwar ulikuwa na athari kubwa katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni na azma na irada thabiti ya viongozi wa muqawama ilikuwa na nafasi kubwa katika kuendeleza mapambano na kusimama imara dhidi ya utawala dhalimu na vamizi wa Kizayuni. 

Akiendelea na ujumbe wake, Ayatullah Khamenei ametilia mkazo pia kwamba kuuawa shahidi viongozi wa muqawama wakiwemo Ismail Haniyeh na al Sinwar hakutasimamisha harakati ya muqawama na kuwa mapambano ya kishujaa ya mashahidi hao yataiweka wazi zaidi njia ya mapambano kwa vijana wa Kipalestina.

Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni sisitizo lake juu ya umuhimu na nafasi ya muqawama katika matukio ya eneo, athari zake na mchango wa jitihada za viongozi wa mapambano ya ukombozi dhidi ya njama za utawala wa Kizayuni na muungaji mkono wake mkuu katika eneo hili yaani Marekani.