FIFA yatakiwa kutoichagua Saudi Arabia kuandaa Kombe la Dunia 2034
(last modified Mon, 11 Nov 2024 12:57:06 GMT )
Nov 11, 2024 12:57 UTC
  • FIFA yatakiwa kutoichagua Saudi Arabia kuandaa Kombe la Dunia 2034

Mashirika ya kutetea haki za binaadamu yamelitaka Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA) kusitisha mchakato wa kuichagua Saudi Arabia kuwa mwenyeji wa michuano ya soka ya Kombe la Dunia mwaka 2034.

Mashirika hayo ya utetezi wa haki za binaadamu ya Amnesty International na Rights Alliance, SRA yamesema hii inatokana na wasiwasi wa ukiukwaji wa haki za binaadamu nchini Saudi Arabia.

Mashirika hayo yametaka kuzuiwa mchakato huo hadi Saudi Arabia itakapotangaza mageuzi makubwa ya haki za binaadamu kabla ya kura hiyo mwezi ujao wa Disemba.

Amnesty na SRA yamesema yamefanya tathmini kuhusu mikakati ya haki za binaadamu iliyopendekezwa na mataifa yaliyoomba kuwa mwenyeji wa michuano hiyo na kuhitimisha katika ripoti mpya kwamba, hakuna pendekezo lililoainisha namna ya kufikia viwango vya haki za binaadamu vinavyotakiwa na FIFA.

Aidha taarifa ya mashirika hayo imesema, kitisho zaidi kiko Saudi Arabia na kwamba michuano hiyo nchini humo ni wazi itakabiliwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za bidaadamu.