Israel yakishambulia kituo cha ulinzi wa raia katika mji wa Gaza
Ndege za kivita za utawala wa Kizayuni zimekishambulia kituo cha ulinzi wa raia katika mji wa Gaza.
Taasisi ya ulinzi wa raia ya Gaza imetangaza kuwa Wazayuni maghasibu kwa mara ya pili wamekishambulia kituo chake kimoja katika mji wa Gaza.
"Mfanyakazi wa kituo hicho na mwanawe pamoja na raia wengine wanne wameuliwa shahidi na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mashambulizi ya ndege za kivita za Israel katika kituo cha ulinzi wa raia huko Gaza.
Taarifa ya taasisi ya ulinzi wa raia katika mji wa Gaza imeongeza kuwa wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wamewafukuza wafanyakazi na wagonjwa katika hospitali ya Indonesia katika Ukanda wa Gaza na sasa wanafanya kila wawezalo kuiharibu kikamilifu hospitali ya Kamal Adwan.
Wagonjwa 90 wamelazwa katika hospitali ya Kamal Adwan katika mazingira magumu sana, na wanajeshi wa Israel wanaendelea kuzuia kuingizwa dawa na chakula katika hospitali hiyo.
Wakati huo huo Shirika la UNRWA linalowahudumia wakimbizi wa Kipalestina limetangaza kuwa kila baada ya saa moja mtoto mmoja anauawa huko Gaza.