Himaya ya wananchi katika Ulimwengu wa Kiislamu kwa muqawama wa Palestina
Mwaka mpya wa Miladia wa 2025 umeanza katika ulimwengu wa Kiislamu kwa himaya na uungaji mkono mkubwa wa wananchi kwa makundi ya wapiganaji wa Palestina na viongozi wa muqawama.
Makundi mbalimbali ya kiraia nchini Jordan na Tunisia yalimiminika mitaani siku ya Jumanne wakati wa mkesha mwaka mpya na kutangaza uungaji mkono wao wa dhati kwa makundi ya wapiganaji wa Palestina na viongozi wa muqawama.
Maandamano makubwa ya raia yalifanyika katika mkesha wa Mwaka Mpya huko Amman, mji mkuu wa Jordan, na karibu na Ubalozi wa Marekani. Katika maandamano hayo, kuendelea uungaji mkono wa Washington kwa utawala wa Kizayuni na kuendelea vita, mauaji na kuzingirwa raia huko Gaza ni mambo ambayo yalilaaniwa na waandamanaji hao.
Wanaharakati na asasi zinazotetea kadhia ya Palestina nchini Tunisia pia walifanya maandamano katika mji mkuu wa nchi hiyo Tunis na kutangaza mshikamano na wananchi madhulumu wa Gaza na kubainisha kuwa, Gaza inakabiliwa na jinai na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni. Aidha waandamanaji hao wamesisitiza kuwa: Katika mazingira haya, kuadhimisha Mwaka Mpya hakuna maana yoyote.
Washiriki wa maandamano hayo wametangaza kuwa, wataendelea kufanya maandamano katika mji mkuu wa Tunisia kuonyesha mshikamano na wananchi wanaodhulumiwa wa Gaza na kuwaunga mkono wananchi wa Palestina, na mikusanyiko hiyo ina mwelekeo mkubwa wa kinembo na kimaadili.
Katika uchunguzi wa maoni wa mtandao wa Rassd wa Misri, shahidi "Yahya Al-Sinwar", aliyekuwa mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina "Hamas", alichaguliwa kama shakhsia wa mwaka 2024 katika ulimwengu wa Kiarabu. Katika uchunguzi huu wa maoni, ambao ulifanyika kwa kushirikisha watumiaji 300,000 wa mtandao huo wa Misri na kwa kura zao, Yahya El-Sanwar alichaguliwa kuwa haiba ya mwaka wa 2024 wa ulimwengu wa Kiarabu kwa 85% ya kura.
Marekani na tawala za Magharibi, katika miaka ya hivi karibuni na hasa baada ya Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa mnamo Oktoba 7, 2023, zimekuwa zikijaribu kwa njia iliyopangwa kujumuisha katika ripoti zao na habari matukio ya vita vya Gaza na mapambano ya makundi ya wapiganaji wa Kipalestina dhidi ya utawala wa Kizayuni.
Kusambaza habari zenye utashi maalumu na kujiepusha na uchapishaji wa ripoti kuhusu mauaji ya halaiki ya utawala wa Kizayuni huko Gaza ni moja ya hatua zilizochukuliwa na mitandao ya habari ya nchi za Magharibi kwa ajili ya kuhadaa maoni ya wananchi hususan Ulaya na Marekani.
Radiamali ya wananchi na mahudhurio makubwa ya wafuasi wa Palestina katika maandamano na matamko ya uungaji mkono kwa makundi ya muqawama wa Palestina na viongozi waliouawa shahidi wa muqawama huo yanaonesha kuwa njama na malengo maovu ya vyombo vya habari vya Marekani na Kizayuni hayajatimia na kwamba, fikra za waliowengi ziko macho nchini Marekani na Ulaya pamoja na ulimwengu wa Kiislamu ambapo kunashuhudiwa kuendelea uungaji mkono kwa watu wa Palestina na malengo yao matukufu.
Kupendwa viongozi wa muqawama kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi wa maoni kunaonyesha chuki na kuchukizwa Waislamu na jinai za utawala wa Kizayuni, na katika hali hii, licha ya propaganda ya Wamagharibi dhidi ya muqawama, lakini taathira ya nafasi ya viongozi mashahidi wa muqawama kwa maoni ya umma katika ulimwengu wa Kiislamu ni kubwa zaidi kuliko hapo awali.