Wapalestina wengine 19 wauawa shahidi
Wapalestina wengine 19 wameuawa shahidi katika muendelezo wa jinai za utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa, jeshi la Kizayuni limefanya jinai nyingine katika Ukanda wa Gaza ambapo watu 19 wameuawa shahidi na wengine 71 kujeruhiwa.
Jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel zinaendelea katika hali ambayo, ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza inazidi kuwa mbaya siku baada ya siku.
Wakati huo huo, hujuma na mashambulio ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza yamesababisha zaidi ya Wapalestina 4,000 kuwa vilema.
Katika ripoti yake ya Jumatano iliyopita, UNICEF ilisema watoto wasiopungua 74 waliuawa katika mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza katika wiki ya kwanza ya mwaka huu mpya wa 2025.
Aidha Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF) umeonya kuwa karibu watoto wote milioni 1.1 katika Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na mgogoro wa afya ya akili na wanahitaji msaada wa kisaikolojia, huku utawala wa Israel ukiendeleza vita vya kikatili dhidi ya wakazi wa eneo hilo linalozingirwa.
Israel ilianzisha vita vya mauaji ya kimbari huko Gaza mnamo Oktoba 7, 2023, baada ya kundi la muqawama la Hamas la Palestina kufanya operesheni ya kihistoria dhidi ya utawala huo ikiwa ni kulipiza kisasi jinai za miongo kadhaa za Wazayuni dhidi ya Wapalestina.