Yemen yaitwanga meli ya kivita ya Marekani kwa mara ya saba
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i121588-yemen_yaitwanga_meli_ya_kivita_ya_marekani_kwa_mara_ya_saba
Msemaji wa Jeshi la Yemen ametangaza kuwa, jeshi la nchi hiyo limefanya operesheni nne za kijeshi dhidi ya utawala wa Kizayuni na Marekani, muhimu zaidi ikiwa ni kuishambulia manuwari ya kubebea ndege ya Marekani iitwayo "Truman" kaskazini mwa Bahari Nyekundu.
(last modified 2025-01-18T03:14:59+00:00 )
Jan 18, 2025 03:14 UTC
  • Yemen yaitwanga meli ya kivita ya Marekani kwa mara ya saba

Msemaji wa Jeshi la Yemen ametangaza kuwa, jeshi la nchi hiyo limefanya operesheni nne za kijeshi dhidi ya utawala wa Kizayuni na Marekani, muhimu zaidi ikiwa ni kuishambulia manuwari ya kubebea ndege ya Marekani iitwayo "Truman" kaskazini mwa Bahari Nyekundu.

Brigedia Jenerali Yahya Saree, ametangaza habari hiyo na kusema kuwa, Jeshi la Yemen limepiga maeneo muhimu ya utawala wa Kizayuni huko "Umm al-Rashrash" kusini mwa ardhi za Palestina zinzokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel.

Jenerali Saree ameongeza kuwa, operesheni hiyo imefanikishwa kwa kutumia makombora manne ya cruise na kupiga shabaha zao kwa umahiri wa hali ya juu.

Msemaji wa Jeshi la Yemen aidha amesema kuwa, kitengo cha ndege zisizo na rubani cha nchi hiyo pia kimefanya operesheni mbili za kijeshi; katika operesheni ya kwanza, droni zake zimepiga maeneo muhimu sana ya utawala katili wa Israel.

Yahya Saree ameendelea kusema: "Operesheni ya pili, imepiga makao muhimu ya jeshi la Israel katika eneo la Ashkelon. Yamepigwa kwa kutumia ndege isiyo na rubani ya Yemen kwa mafanikio makubwa." 

Msemaji wa Vikosi vya Ulinzi vya Yemen amebainisha kuwa operesheni hizo tatu zimeambatana na operesheni nyingine iliyofanywa na Jeshi la Wanamaji la Yemen, wakati manuwari ya kubebea ndege ya Marekani iitwayo "Truman" iliposhambuliwa na Jeshi la Yemen, kaskazini mwa Bahari Nyekundu.

Yahya Saree pia alisema: "Shambulio dhidi ya meli ya kivita ya Marekani limefanywa kwa kutumia droni kadhaa na hiyo ni mara ya saba kwa jeshi letu la Yemen kupiga manuwari ya Marekani kwenye Bahari ya Sham."

Msemaji wa Jeshi la Yemen vilevile amesema: "Tuko tayari kwa hatua au mvutano wowote na Marekani na utawala wa Kizayuni, na tunafuatilia kwa karibu hali ya Ghaza. Ikiwa adui hatoheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano au kufanya operesheni dhidi ya wananchi wa Palestina huko Ghaza, sisi nasi tutaiadhibu Israel kwa namna tutakavyoona inafaa zaidi." 

Jenerali Saree amemalizia kwa kusema: "Tunawaambia wananchi wa taifa la Palestina na wanamapambano wote kwamba tutaendelea kuwa pamoja nao. Kamwe hatutoiacha Palestina peke yake wala kuitekeleza kadhia yake, hadi pale ardhi za Palestina zitakapokombolewa kikamilifu na kutimuliwa humo utawala wa Kizayuni."