Kimbunga cha al-Aqsa chamsomba Mkuu wa Majeshi ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i121740-kimbunga_cha_al_aqsa_chamsomba_mkuu_wa_majeshi_ya_israel
Mkuu wa Vikosi vya Majeshi ya Israel, Herzi Halevi ametangaza kujiuzulu kufuatia kushindwa kwake kuzima Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa dhidi ya utawala huo haramu.
(last modified 2025-01-21T23:56:52+00:00 )
Jan 21, 2025 23:56 UTC
  • Kimbunga cha al-Aqsa chamsomba Mkuu wa Majeshi ya Israel

Mkuu wa Vikosi vya Majeshi ya Israel, Herzi Halevi ametangaza kujiuzulu kufuatia kushindwa kwake kuzima Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa dhidi ya utawala huo haramu.

Akitangaza kujiuzulu jana Jumanne, Halevi amekiri kushindwa kwake kijeshi kuzuia Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa iliyowafanywa na wanamuqawama wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas mnamo Oktoba 7, 2023.

Mkuu huyo wa Majeshi ya Kizayuni amesema kwamba tayari amewajulisha Waziri Mkuu wa utawala huo haramu, Benjamin Netanyahu na Waziri wa Vita, Israel Katz juu ya uamuzi wake wa kujiuzulu kuanzia Machi 6, wakati muhula wake wa miaka mitatu utakapofikia tamati.

Utawala wa Kizayuni wa Israel ulishindwa vibaya kijeshi na kijasusi na Harakati ya Muqawama ya Hamas wakati wa Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa, iliyofanywa kwa shabaha ya kukabiliana na uvamizi wa Israel uliodumu kwa miongo kadhaa huko Palestina.

Si vibaya kuashiria hapa kuwa, Novemba mwaka jana, Mkuu huyo wa Majeshi ya Israel alikoswakoswa katika hujuma ya makombora ya wapiganaji wa Hamas huko kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.

Baada ya vita vya miezi 15, na kuuawa shahidi zaidi ya raia 46,000 wa Kipalestina tangu Oktoba 7, 2023, utawala katili wa Israel bila ya kufikia malengo yake hatimaye ulilazimika kukubali makubaliano ya kusitisha mapigano na Hamas.