Israel yaendelea kumwaga damu za Wapalestina Ukingo wa Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i121794-israel_yaendelea_kumwaga_damu_za_wapalestina_ukingo_wa_magharibi
Wanajeshi wa Israel wamewaua shahidi Wapalestina wengine wawili katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan linalokaliwa kwa mabavu, wakati wakiendelea na kampeni ya kijeshi ambayo imeifanya kambi ya wakimbizi ya Jenin "kutoweza kukalika".
(last modified 2025-01-23T04:19:48+00:00 )
Jan 23, 2025 04:19 UTC
  • Israel yaendelea kumwaga damu za Wapalestina Ukingo wa Magharibi

Wanajeshi wa Israel wamewaua shahidi Wapalestina wengine wawili katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan linalokaliwa kwa mabavu, wakati wakiendelea na kampeni ya kijeshi ambayo imeifanya kambi ya wakimbizi ya Jenin "kutoweza kukalika".

Taarifa ya Brigedi za Izzuddin al-Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, imethibitisha kuuawa shahidi kwa wapiganaji wawili wa kikosi hicho.

Qassam imewataja wawili hao kuwa ni Qutaiba al-Shalabi na Mohammed Nazal, ambao wameuawa shahidi na vikosi vya Israeli katika mji wa Burqin katika mkoa wa Jenin. Kwa mujibu wa shirika la habari la Wafa, miili ya al-Shalabi, 30, na Nazal, 25, ingali inashikiliwa na Wazayuni.

Wanajeshi makatili wa utawala wa Kizayuni juzi Jumanne walivamia mji wa Jenin na kuwauwa shahidi Wapalestina wasiopungua kumi na kujeruhi makumi ya wengine.

Haya yanajiri huku Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu katika ardhi za Palestina akitahadharisha kuwa mauaji ya kimbari ya Israel yanaweza kupanuka kutoka Gaza hadi Ukingo wa Magharibi, kwa kuzingatia operesheni kubwa ya kijeshi inayoendelea kufanywa na utawala huo ghasibu katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Jenin.

Francesca Albanese alieleza haya jana huku Israel ikiendeleza hujuma za kikatili dhidi ya Wpalestina katika eneo la Ukingo wa Magahribi tangu kuanza kutekelezwa makubaliano ya kusitisha mapigano Ukanda wa Gaza, siku ya Jumapili.