Israel yaifungisha virago UNRWA, yataka iondoke Quds kufikia Januari 30
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i121888-israel_yaifungisha_virago_unrwa_yataka_iondoke_quds_kufikia_januari_30
Utawala wa Kizayuni wa Israel umesema kuwa, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) lina hadi mwisho wa mwezi huu wa Januari kuondoka katika mji mtukufu wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu.
(last modified 2025-01-25T08:04:25+00:00 )
Jan 25, 2025 08:04 UTC
  • Israel yaifungisha virago UNRWA, yataka iondoke Quds kufikia Januari 30

Utawala wa Kizayuni wa Israel umesema kuwa, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) lina hadi mwisho wa mwezi huu wa Januari kuondoka katika mji mtukufu wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu.

Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa, Danny Danon amesema katika barua yake ya jana Ijumaa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres kwamba, "UNRWA lazima isitishe shughuli zake huko Jerusalem (Quds), na kuhama majengo yote ambayo inafanyia kazi katika jiji hilo, kabla ya Januari 30, 2025."

Utawala haramu wa Israel umehalalisha hatua yake hiyo kwa kuibua madai yasiyo na msingi kwamba, UNRWA, ambayo imekuwa ikiwaunga mkono Wapalestina tangu 1949, eti inaajiri wafanyakazi wanaoshiriki katika shughuli za kigaidi.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina limekuwa likisisitiza kuwa, hakuna taasisi yoyote inayoweza kujaza nafasi ya shirika hilo katika kuwahudumia na kuwafikishia misaada wakimbizi wa Kipalestina.

UNRWA ndilo shirika kubwa zaidi la misaada ya kibinadamu kwenye Ukanda wa Gaza ambalo lilikuwa na takriban wafanyakazi 13,000 kabla ya utawala wa Kizayuni kuanzisha jinai za kutisha kwenye ukanda huo Oktoba mwaka 2023.

Oktoba mwaka jana 2024, bunge la Israel (Knesset) lilipasisha muswada wa kupiga marufuku shughuli zote za shirika hilo la Umoja wa Mataifa.

Mapema mwezi huu, Philip Lazzarini, Kamishna Mkuu wa Shirika la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) alisema kuwa, kuundwa kwa taifa huru la Palestina ndio suluhisho la matatizo ya eneo hilo.