Ansarullah: Israel inatumia uungaji mkono wa US kukiuka makubaliano
(last modified Sat, 01 Mar 2025 07:13:53 GMT )
Mar 01, 2025 07:13 UTC
  • Ansarullah: Israel inatumia uungaji mkono wa US kukiuka makubaliano

Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema Yemen inafuatilia kwa karibu utekelezwaji wa makubaliano ya usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza na kuongeza kuwa, inashuhudia namna "adui Mzayuni" anakwepa kutekeleza majukumu yake.

Abdul Malik al-Houthi amesema, "Utawala wa Kizayuni unatumia uungaji mkono wa Marekani kukiuka makubaliano."

Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa al-Maseera, al-Houthi amesema kuwa, kushindwa adui kujitoa katika mhimili wa Rafah ni ukiukaji wa wazi wa mikataba ya huko nyuma kati ya Misri na adui Mzayuni.

Ameonegeza kwa kusema, "Kushindwa kwa wavamizi kujiondoa katika mhimili wa Rafah ni tishio hatari kwa taifa la Palestina na serikali na jeshi la Misri."

Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesisitiza kwamba "adui" hajatekeleza sehemu kubwa ya majukumu yake, hasa kuhusu suala la kibinadamu, na pia anaepuka kutekeleza majukumu yake mengine, ikiwa ni pamoja na kujiondoa kutoka kwenye mhimili wa Rafah. Al-Houthi amebainisha kuwa, Israel haijajiondoa kabisa kutoka kusini mwa Lebanon, na huu ni uvamizi na tishio kwa taifa la Lebanon na ukiukaji wa uhuru na mamlaka ya kujitawala Lebanon.

Abdul Malik al-Houthi ameeleza bayana kuwa, utawala wa Kizayuni unasonga mbele katika majimbo matatu ya kusini mwa Syria na unakalia kwa mabavu maeneo mengi zaidi kila kuchao.

Kiongozi huyo wa Ansarullah ya Yemena ameonya kuwa, “Adui Mzayuni na Marekani wanajaribu kuhalalisha ukiukaji wa haki za Umma wa Kiislamu, na wanatarajia kwamba hakuna atakayejibu uchokozi wao na kukabiliana nao."