Hamas: Maisha ya mateka wa Israel si muhimu kwa Netanyahu
(last modified Fri, 16 May 2025 02:21:00 GMT )
May 16, 2025 02:21 UTC
  • Hamas: Maisha ya mateka wa Israel si muhimu kwa Netanyahu

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetilia mkazo masharti yake makuu kuhusu makubaliano ya kudumu ya kusimamisha vita na kuondoka kikamilifu wanajeshi vamizi wa Israel kwenye Ukanda wa Ghaza ikitangaza kuwa, Netanyahu amefeli katika njama zake za kufikia makubaliano bila ya kusitisha vita kikamilifu na kwamba mateka wa Kizayuni si muhimu kwa Netanyahu.

Hayo yamo kwenye taarifa mpya ya HAMAS ambayo imeongeza kuwa, "Utawala wa Kizayuni unaendeleza jinai zake dhidi ya wananchi wa Ukanda wa Ghaza, unakwamisha juhudi za wapatanishi, na Netanyahu anataka vita licha ya kujua kwamba havina mwisho, lakini aelewe kwamba bila ya kufuatwa masharti ya Muqawama, hakuna mateka watakaoachiliwa huru." Taarifa ya HAMAS aidha imesema: "Wakati wapatanishi wakifanya juhudi nyingi za kurejesha mchakato wa mazungumzo, Wazayuni wavamizi wanakwamisha juhudi hizo kwa kutoa mashinikizo ya kijeshi kwa raia wasio na hatia kupitia mashambulizi yaliyoenea kona zote na kuwasababishia mateso zaidi watu wetu, lakini hilo ni jaribio la utawala wa Kizayuni uliokata tamaa."

HAMAS imeongeza kuwa: Sisitizo la baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni la kutaka kufanya mazungumzo na kufikia makubaliano bila ya kusimamishwa vita na kuendelea kupuuza juhudi za wapatanishi, linadhihirisha asili ya fikra za kijinai za utawala huo. Taarifa hiyo vilevile imesema: "Ulimwengu mzima unataka kuona vita vinamalizika Ghaza lakini Netanyahu anataka vita visivyoisha na hajali hatima ya mateka wa Kizayuni walioko Ghaza. Imesema: "Netanyahu hajali kabisa maisha na usalama wa mateka wa Kizayuni, na kwa mauaji na jinai zake, amethibitisha kwamba yeye si tishio tu kwa wananchi wa Palestina, bali pia ni hatari halisi kwa eneo hili zima na dunia nzima.