Je, dunia mara hii ina nia ya kufanikisha kuasisiwa nchi huru ya Palestina?
Katika hatua ya kihistoria, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepasisha azimio lililopendekezwa na Ufaransa na Saudi Arabia, na kutangaza kuunga mkono kuanzishwa kwa nchi huru la Palestina na kutekelezwa njia ya ufumbuzi wa serikali mbili.
Azimio lililopendekezwa na Ufaransa na Saudi Arabia ambalo linasisitiza kuanzishwa nchi huru ya Palestina limepiitishwa kwa kura za ndio 142 na 10 za hapana.
Kupitishwa kwa azimio ambalo linatambua rasmi kuasisiwa nchi huru ya Palestina huku Israel ikiendeleza jinai zake katika Ukanda wa Gaza, kunaonyesha kufikiwa muafaka wa kimataifa ya dhidi ya uvamizi na ukiukaji wa haki za binadamu kunakofanywa na Israel. Hatua hii pia inaakisi mabadiliko muhimu katika sera za kimataifa na nafasi ya Palestina katika milinganyo ya kimataifa. Hasa ikizingatiwa kuwa kupasishwa azimio hili tajwa licha ya kupingwa na nchi kama Marekani ni hatua chanya kuelekea kurejeshwa haki za Wapalestina na kufikia amani ya kudumu katika eneo la Mashariki ya Kati.
Azimio jipya la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanzakwa upande moja limeunga mkono pakubwa kuundwa nchi huru ya Palestina na katika upande mwingine, limeashiria kuanzishwa mchakato wa amani wenye itibari kwa ajili ya kutatua kadhia ya Palestina na Israel. Lengo kuu la azimio hilo ni kupatikana njia ya ufumbuzi ambayo serikali ya Palestina itatambuliwa rasmi kama nchi huru.
Kuongezeka mashinikizo ya kidiplomasia dhidi ya Israel, kudhoofika nafasi ya Israel kimataifa, kupanda juu nafasi ya Palestina katika majukwaa ya kimataifa, kuongezeka mashinikizo ya kimataifa kwa lengo la kushughukila kadhia ya Palestina na kukomeshwa vita na mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Gaza na katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni kati ya malengo mengine ya kupasishwa azimio hili.
Katika upande mwingine, baada ya miaka kadhaa ya mapigano na kujiri maafa ya binadamu huko Palestina, kupasishwa azimio la kutambua kuundwa taifa huru la Palestina kunaashiria kujiri mabadiliko katika mitazamo ya nchi nyingi duniani kuhusu kadhia ya Palestina.
Hatua hii tajwa ni ishara ya kimataifa kwa nchi zinazoihami na kuiunga mkono Israel, na inatuma ujumbe huu kwamba, wakati umefika sasa wa kutoa jibu chanya kwa matakwa ya Wapalestina na kutafuta suluhu za kisiasa badala ya kuendeleza hali ya mchafukoge.
Nchi za Ulaya ambazo kwa miaka kadhaa sasa zinaiunga mkono Israe hivi sasa zimelazimika kuchukua za kivitendo kutokana na chokochoko na hatua za uvamizi za utawala wa Kizayuni na mashinikizo ya fikra za waliowengi duniani. Kuunga mkono azimio la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuanzishwa nchi huru ya Palestina ni mfano wa mabadiliko haya ya misimamo.
Pamoja na haya yote, kupasishwa azimio hili na Baraza Kuu la UN kumepingwa na Marekani na Israel. Morgan Ortagus, Mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amelitaja azimio hilo wakati wa kupigiwa kura kuwa ni tishio kwa usalama wa Israel na "kifo kwa muundo wa idadi ya watu wa Israel. Amesisitiza kuwa kupasishwa azimio kama hilo kutasaidia tu kuimarisha makundi yenye itikadi kali na kuvuruga mchakato wa amani. Israel pia imepinga uamuzi huu na kulitaja azimio hilo kuwa halifai na lisilo na taathira.
Ni wazi kuwa kupitishwa kwa azimio hili katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kunaonyesha uungaji mkono mkubwa kwa suluhisho la upatikanaji wa serikali mbili na kuassi nchi ya Palestina. Hatua hii ambayo imechukuliwa hasa katika hali ambayo haki za Wapalestina zinaendelea kukiukwa pakubwa huku Israel ikishadidsha jinai zake huko Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni hatua kubwa na ya jadi inayoweza kuhesabiwa kama njia muhimu ya utatuzi kwa ajili ya kuishinikiza Israel ibadili mtazamo wake na kusitisha hujuma zake kijeshi na ukiukaji wa haki za binadamu.