Mkuu wa Daesh taabani baada ya kupewa sumu
Mkuu wa kundi la kigiaid la ISIS (Daesh), Ibrahim al-Samarrai, maarufu kama Abu Bakr al-Bahgdadi, ameripotiwa kuwa katika hali mbaya ya kiafya baada ya kuwekewa sumu katika chakula chake.
Shirika la habari la Iraq limeripoti kuwa, chakula kilichoandaliwa kwa ajili ya al-Baghdadi na makamanda wengine watatu wa ngazi za juu wa Daesh katika wilaya ya Beaaj, kusini magharibi mwa mkoa wa Nineveh kilikuwa na sumu na kuwasababishia wanne hao maumivu makali ya tumbo.
Duru za habari zimedokeza kuwa, kundi hilo la kitakfiri limeanzisha uchunguzi ili kubaini wahusika wa kitendo hicho.
Itakumbukwa kuwa, mwezi Juni mwaka huu, al-Bahgdadi alijeruhiwa katika hujuma ya ndege za kivita, magharibi mwa mkoa wa Ninevah, karibu na mpaka wa Syria.
Al-Baghdadi alijitangaza kuwa mkuu wa kundi hilo la ISIS mwaka 2014 wakati kundi hilo lilipoyadhibiti maeneo mengi ya Iraq na Syria. Hata hivyo katika miezi ya hivi karibuni magaidi wa ISIS wamepata pigo kubwa sana katika nchi hizo mbili ambapo wanajeshi wa nchi hizo wanaendelea kukomboa ardhi zilizokuwa zimetekwa na kundi hilo la wakufurishaji.