Dec 03, 2016 07:51 UTC
  • Waziri Mkuu wa Iraq: Ushindi dhidi ya DAESH unakaribia

Waziri Mkuu wa Iraq Haidar al-Abadi amesema, kutokana na kusonga mbele vikosi vya pamoja vya nchi hiyo katika pande zote za medani ya vita kwa ajili ya kuukomboa mji wa Mosul kutoka kwenye makucha ya kundi la kigaidi la kitakfiri na Daesh, ushindi wa jeshi la nchi hiyo uko karibu mno kupatikana.

Taarifa iliyotolewa jana na ofisi ya Waziri Mkuu wa Iraq ambaye pia ni Kamanda Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo imeashiria hasara kubwa mno liliyopata kundi la kigaidi la Daesh katika operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul na kubainisha kwamba Haidar al-Abadi ameandaa mikakati kadhaa kwa ajili ya kuongeza kasi ya operesheni ya kuukomboa mji huo.

Mnamo siku ya Jumanne pia Waziri Mkuu wa Iraq alitangaza katika kikao cha kila wiki na waandishi wa habari mjini Baghdad kuwa: "Leo Iraq inakaribia kufikia umoja kuliko wakati wowote ule, na hivi sasa kila raia wa Iraq anafanya jitihada za kulinda ardhi ya nchi yake."

Wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh

Kuanzia tarehe 17 Oktoba mwaka huu, vikosi vya pamoja vya ulinzi vya Iraq vinavyojumuisha jeshi, vikosi vya kujitolea vya wananchi, vikosi vya Kikurdi vya Peshmarga pamoja na Polisi ya Taifa, huku vikisaidiwa na vikosi vya anga vya jeshi la nchi hiyo, vilianzisha operesheni za mashambulio ya kuukomboa mji wa Mosul ambao ni makao makuu ya mkoa wa Nainawa kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, ambapo hadi sasa vimefanikiwa kupata ushindi mkubwa.

Mji wa Mosul ulivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Daesh mwezi Juni mwaka 2014.../

 

Tags