Intifadha; kielelezo kikuu cha kisiasa Palestina
Katika hali ambayo imepita miaka 29 tangu kulipotokea Intifadha ya Kwanza huko Palestina, harakati hiyo ya wananchi wanamuqawama imeendelea kuhesabiwa kuwa kielekezo kikuu cha kisiasa huko Palestina
Disemba 8 mwaka 1987 yaani miaka 29 iliyopita, kulitokea Intifadha ya Kwanza dhidi ya utawala haramu wa Israel iliyojulikana kwa jina la Intifadha ya Mawe, ambayo ilianzia kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza. Sababu ya kutokea Intifadha hiyo ni kukanyagwa na gari la Israel vibarua kadhaa wa Kipalestina katika kituo cha upekuzi cha Beit Hanoun na kupelekea Wapalestina wanne kuuawa shahidi. Intifadha ya Pili ya Palestina iliyojulikana kwa jina la Intifadha ya al-Aqswa ilianza Disemba 28 mwaka 2000. Chanzo cha Intifadha hiyo ilikuwa ni hatua ya kifedhuli ya Waziri Mkuu wa wakati huo Ariel Sharon ya kulinajisi eneo takatifu la Waislamu kwa kuingia katika Masjidul Aqswa akiwa pamoja na wanajeshi wa Israel.
Aidha Intifadha ya Tatu, inayojulikana kwa jina la Intifadha ya Quds, cheche za moto wake zilianza tarehe 24 Septemba mwaka jana siku ambayo ilisadifiana na maadhimisho ya Sikukuu ya Eid al-Adh'ha ya Waislamu na sikuu ya Ghufran ya Mayahudi. Sababu ya kutokea Intifadha hiyo ni hatua ya Waziri wa Kilimo wa Israel aliyefuatana na walowezi wa Kiyahudi kuingia katika msikiti wa al-Aqswa.
Hata hivyo waziri huyo na walowezi hao walikabiliwa upinzani wa waumini wa Kiislamu waliokuwemo msikitini humo kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Swala ambao walifanya kila wawezalo kuwazuia.

Wanajeshi wa Israel waliwashambulia waumini hao kwa risasi za plastiki pamoja na gesi za kutoa machozi. Wapalestina wengi walijeruhiwa katika jinai hiyo. Pamoja na hayo, Intifadha ya Quds ilianza tarehe Mosi Oktoba mwaka jana kwani katika siku hiyo kijana Muhannad Halabi aliuawa shahidi baada ya kufanya operesheni ya kishujaa ya kujitolea kufa shahidi dhidi ya wanajeshi wa Israel.
Tukiachilia mbali sababu tofauti za kuanza Intifadha za Palestina, kuna tofauti nyingine pia zinazohusiana na Intifadha hizo. Katika Intifadha ya Mawe takribani Wapalestina 1300 waliuawa shahidi. Wapalestina 4412 waliuawa shahidi katika Intifadha ya al-Aqswa na hadi sasa Wapalestina 268 wameshauawa shahidi tangu ilipoanza Intifadha ya Quds. Intifadha ya Mawe ilidumu kwa muda wa miaka 6. Intifadha ya al-Aqswa ilidumu kwa muda wa miaka 5 kuanzia mwaka 2000 hadi 2005 huku Intifadha ya Quds iliyoanza mwaka jana ikiingia mwaka wake wa pili hivi sasa.
Intifadha ya Mawe ilianzia Ukanda wa Ghaza. Intifadha mbili za al-Aqswa na Quds zimeanzia katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Jambo hilo linabainisha ukweli kwamba, mapambano ya Wapalestina dhidi ya utawala vamizi wa Israel hayaishii tu katika Ukanda wa Ghaza bali Wapalestina wote wanashiriki katika mapambano hayo popote walipo.

Kwa maneno mengine ni kuwa, katika hali ambayo makundi ya Palestina yanatofautiana kuhusiana na namna ya kukabiliana na utawala haramu wa Israel, wananchi wa ardhi hizo wana mtazamo mmoja ambapo sambamba na kupinga kuweko mapatano ya aina yoyote na Israel wanatambua kuwa, kuendesha mapambano dhidi ya utawala huo vamizi ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele kikubwa. Nukta nyingine ni kwamba, kiwango cha uungaji mkono wa nchi za Kiarabu kwa Intifadha za Palestina kimekuwa kikipungua siku baada ya siku.
Katika Intifadha ya Mawe nchi nyingi za Kiarabu ziliiunga mkono lakini idadi ya nchi zilizounga mkono Intifadha ya al-Aqswa ilipungua. Katika Intifadha ya hivi sasa ya Quds si tu kwamba, nchi za Kiarabu haziiungi mkono, bali kwa namna fulani zimekuwa pamoja na Israel kuikandamiza. Moja ya nukta za pamoja za Intifadha Tatu za Palestina ambayo tunaweza kuiashiria hapa ni kwamba, nyenzo za mapambano za wananchi wa Palestina dhidi ya wanajeshi wa Israel hazijabadilika, kwani mawe yameendelea kuwa wenzo na silaha muhimu ya Intifadha.