Misri yarefusha muda wa uingiliaji wake kijeshi Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i24095-misri_yarefusha_muda_wa_uingiliaji_wake_kijeshi_yemen
Ofisi ya rais wa Misri ilitangaza jana Jumapili kwamba Baraza la Ulinzi wa Kitaifa la nchi hiyo limerefusha muda wa askari jeshi wa nchi hiyo kuendelea kuhudumu katika muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia dhidi ya Yemen.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Jan 23, 2017 03:31 UTC
  • Misri yarefusha muda wa uingiliaji wake kijeshi Yemen

Ofisi ya rais wa Misri ilitangaza jana Jumapili kwamba Baraza la Ulinzi wa Kitaifa la nchi hiyo limerefusha muda wa askari jeshi wa nchi hiyo kuendelea kuhudumu katika muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia dhidi ya Yemen.

Taarifa iliyotolewa na baraza hilo mwishoni mwa kikao chake inasema kuwa serikali ya Misri imeamua kurefusha muda wa askari hao kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kulinda usalama wa kitaifa wa nchi hiyo na nchi nyingine za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi katika bahari ya Sham na eneo la Babul Mandab. Haikufahamika mara moja muda huo umerefushwa hadi lini. Muda wa kuhudumu askari jeshi wa Misri katika muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia umerefushwa katika hali ambayo uhusiano wa nchi mbili hizo kuhusiana na mgogoro wa Syria umeharibika sana katika siku za hivi karibuni.

Maafa na uharibifu unaosababishwa na hujuma ya kijeshi ya Saudia nchini Yemen ni mkubwa

Uhusiano huo umevurugika zaidi kufuatia uamuzi uliotolewa hivi karibuni na mahakama kuu ya Misri kuhusiana na visiwa viwili vya nchi hiyo vilivyokuwa vimekabidhiwa kwa Saudi Arabia. Saudia imekuwa ikiongoza hujuma ya muungano wa kijeshi dhidi ya Yemen tokea mwezi Machi 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani rais mtoro wa nchi hiyo Abdu Rabbuh Mansur Hadi ambaye ni kibaraka wa utawala wa Riyadh, hujuma ambayo hadi sasa imepelekea makumi ya maelfu ya raia wa Yemen kupoteza maisha na kujeruhiwa, wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake wasio na hatia yoyote. Hujuma hiyo vilevile imepelekea nchi masikini ya Yemen kukabiliwa na mgogoro mkubwa wa uhaba wa madawa, chakula na kuenea kwa magonjwa mbalimbali nchini.