Taarifa ya Astana yasisitiza mapambano dhidi ya ugaidi nchini Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i24195-taarifa_ya_astana_yasisitiza_mapambano_dhidi_ya_ugaidi_nchini_syria
Pande zilizoshiriki katika mkutano wa amani nchini Syria katika mji mkuu wa Kazakhstan, Astana zimetoa taarifa ya mwisho inayosisitiza udharura wa kulindwa ardhi yote ya Syria na kudumishwa mapambano dhidi ya ugaidi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 24, 2017 14:59 UTC
  • Taarifa ya Astana yasisitiza mapambano dhidi ya ugaidi nchini Syria

Pande zilizoshiriki katika mkutano wa amani nchini Syria katika mji mkuu wa Kazakhstan, Astana zimetoa taarifa ya mwisho inayosisitiza udharura wa kulindwa ardhi yote ya Syria na kudumishwa mapambano dhidi ya ugaidi.

Taarifa hiyo ambayo imesomwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kazakhstan, Kairat Abdrakhmanov imesema kuwa, mazungumzo hayo ni utangulizi wa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya serikali ya Syria na wapinzani wake.

Taarifa hiyo imesema, pande zote katika mazungumzo hayo zimeahidi kudumisha mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi kama Daesh na Jabhatu Nusra. (Fat'hu Sham). Taarifa ya mkutano wa Astana imesema, mazungumzo yajayo huko Geneva kuhusu amani nchini Syria yanapasa kuanza haraka na kwa mujibu wa maazimio ya kimataifa tena kwa kushirikisha makundi yote ya upinzani. 

Taarifa hiyo pia imetilia mkazo udharura wa kulindwa ardhi yote ya Syria na kusema, vita na mapigano nchini Syria vinapaswa kukomeshwa kwa mujibu wa azimio nambari 2254 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kutayarisha mazingira mazuri ya kufikisha misaada ya kibinadamu kwa watu walioathiriwa na vita. 

Mkutano wa amani wa Astana

Hata hivyo taarifa ya Astana imesema vita havitasimamishwa katika maeneo ya Syria yanayodhibitiwa na makundi ya kigaidi kama Daesh na Jabhatu Nusra. 

Mazungumzo ya kujadili njia za kurejesha amani nchini Syria yalianza Jumatatu ya jana katika mji mkuu wa Kazakhstan, Astana yakizishirikisha serikali na kambi ya upinzani nchini Syria kwa ubunifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia na Uturuki.