Hatua nyingine muhimu kuelekea ukombozi kamili wa Mosul
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i25566-hatua_nyingine_muhimu_kuelekea_ukombozi_kamili_wa_mosul
Jeshi la Iraq limeendeleza operesheni ya kukomboa eneo la magharibi mwa Mosul kwa kudhibiti uwanja wa ndege wa mji huo kutoka kwenye makucha ya wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 24, 2017 04:39 UTC
  • Hatua nyingine muhimu kuelekea ukombozi kamili wa Mosul

Jeshi la Iraq limeendeleza operesheni ya kukomboa eneo la magharibi mwa Mosul kwa kudhibiti uwanja wa ndege wa mji huo kutoka kwenye makucha ya wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh.

Ripoti ya televisheni ya taifa ya Iraq imesema kuwa, jeshi la nchi hiyo limeingia katika uwanja wa ndege wa Mosul na kuukomboa kutoka kwenye udhibiti wa Daesh. 

Mafanikio hayo yamepatikana baada ya siku tano tu tangu kuanza kwa operesheni ya kukomboa uwanja huo. Kukombolewa uwanja wa ndege wa Mosul ni hatua muhimu katika mapambano ya kukomboa kikamilifu mji wa Mosul kwa sababu ndege za kivita za Iraq sasa zitaanza kutumia uwanja huo katika operesheni zake za kivita na kwa ajili ya kuharakisha ukombozi wa kambi ya Ghazlani.

Operesheni kubwa ya kukomboa eneo la magharibi mwa Mosul kutoka kwa kundi la kigaidi la Daesh inashirikisha askari karibu laki moja na maudhui muhimu katika operesheni hiyo ni jinsi ya kugawana majukumu ya utekelezaji wake. Kwa mfano tu jukumu la kukomboa uwanja wa ndege wa mji huo ni la Kikosi cha Radiamali ya Haraka cha Jeshi na Polisi ya Federali ya Iraq vikisaidiwa na Jeshi la Anga na Kikosi cha Mizinga, huku Kikosi cha Kupambana na Ugaidi kikipewa kazi ya kukomboa kambi ya al Ghazlani. Ukombozi wa kambi la al Ghazlani utaliwezesha jeshi la Iraq kudhibiti njia za mawasiliano kusini mwa Mosul. Udhibiti wa njia hizo ni miongoni mwa statijia muhimu sana kwa sababu utasaidia kuzidisha mzingiro dhidi ya wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh. 

Jeshi la Iraq baada ya kukomboa uwanja wa ndege wa Mosul

Ushahidi unaonesha kuwa, magaidi wa kundi la Daesh kwa sasa wanazingirwa na jeshi la Iraq katika eneo la magharibi mwa Mosul. Hivyo ili kuweza kuvunja mzingiro huo na kurefusha mapigano, magaidi hao wanatumia stratijia ya kutumia raia wa mji huo kama ngao ya kujikinga na vita na mashambulizi ya jeshi la Iraq. Mbinu hiyo hiyo pia ilitumiwa na magaidi hao wakati wa operesheni ya jeshi la Iraq ya kukomboa eneo la al Anbar.

Utumiaji wa raia kama ngao ya vita katika operesheni ya kukomboa eneo la magharibi mwa Mosul unaweza kusababisha maafa makubwa hasa kwa kutilia maana muundo wa jamii ya eneo hilo na idadi ya watu wake. Mitaa na barabara za eneo la magharibi mwa Mosul ni nyembamba sana na linasifika kwa kuwa na idadi kubwa ya watu. Sifa hizo mbili zinazidisha uwezekano wa kutokea maafa makubwa kutokana na stratijia ya Daesh ya kutumia raia kama ngao ya binadamu ya kujikinga na mashambulizi ya jeshi la Iraq. 

Daesh wakijitayarisha kuchinja raia.. 

Katika uwanja huo, Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu hali mbaya ya maelfu ya raia wa Mosul.

Alaa kulli hal, magaidi wa Daesh wanaelewa vyema kwamba, kukombolewa eneo la magharibi mwa Mosul kutakuwa na maana ya kutoweka na kuyoyoma ndoto ya kundi hilo la kigaidi ya kuasisi dola eti la khilafa katika ardhi ya Iraq.