Marekani yaongeza idadi ya wanajeshi wake ndani ya Syria
Vyombo vya habari vya Syria vimetangaza kuwa, Marekani imetuma karibu wanajeshi wengine 200 katika kijiji cha al Asaliyyah, kaskazini magharibi mwa mji wa Manbij, wa kaskazini mwa Syria.
Shirika la habari la IRNA limezinukuu duru za Syria zikitangaza habari hiyo leo na kuongeza kuwa, kwa kutumwa wanajeshi hao wapya huko Syria kunaifanya idadi ya wanajeshi wa Marekani walioko ndani ya ardhi ya Syria kufikia 700.
Wakati huo huo kundi linalojiita la kusimamia haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake makuu nchini Uingereza na ambalo liko karibu na magenge ya kigaidi nchini Syria limetangaza kuwa, vifaru na magari ya deraya 43 ya Marekani yamefika katika viunga vya mji wa Manbij na inadaiwa kuwa lengo la kutumwa na wanajeshi hao eti ni kupambana na magaidi wa Daesh (ISIS).
Marekani kwa kushirikiana na Saudi Arabia, Uturuki, Qatar na utawala wa Kizayuni wa Israel zinayasaidia magenge yanayofanya jinai na mauaji dhidi ya raia na maafisa wa serikali ya Syria kwa miaka kadhaa sasa.
Rais Bashar al Assad wa Syria jana alitangaza rasmi kuwa, askari yeyote anayeingia ndani ya ardhi ya nchi hiyo bila ya idhini ya serikali ya Damascus anahesabiwa kuwa ni mvamizi na kuzitaka Marekani na Uturuki ziondoe mara moja wanajeshi wao vamizi ndani ya ardhi ya Syria.
Jeshi la Syria na waitifaki wake wamepata ushindi mkubwa sana dhidi ya magenge ya kigaidi na inaonekana wazi kwamba waungaji mkono wa magenge hayo ya kihalifu na kitakfiri kama vile Marekani, Uturuki na Saudi Arabia hawafurahishwi hata kidogo na ushindi huo wa jeshi la Syria.