Miripuko ya mabomu; natija ya kushindwa mazungumzo ya Syria
Katika hali ambayo hata mazungumzo ya Astana 3 kuhusiana na mgogoro wa Syria nayo yameshindwa, mashambulizi ya mabomu ya magenge ya kigaidi yanayopata uungaji mkono wa madola ya kigeni yameonesha wazi kuwa magenge hayo hayapendi kuona utulivu unarejea nchini humo.
Siku ya Jumatano na baada ya kupita muda mrefu wa utulivu, Damascus, mji mkuu wa Syria ulikumbwa na miripuko mingine ya kigaidi. Mkahawa wa bustani moja pamoja na wizara ya mahakama ya Syria ni maeneo yaliyolengwa na magaidi kwenye mashambulizi yao hayo. Watu wasiopungua 34 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa kwenye miripuko hiyo. Jumatatu iliyopita pia, miripuko miwili ya mabomu iliyotokea mjini Damascus iliua wafanya ziara 74 wengi wao wakiwa ni raia wa Iraq na kujeruhi makumi ya wengine.
Wachambuzi wa mambo wanatoa tathmini tofauti kuhusu sababu za kutokea miripuko hiyo ya hivi karibuni mjini Damascus. Moja ya sababu zake kuu ni kushindwa mazungumzo ya amani ya Astana na Geneva. Baada ya mazungumzo ya Astana 1 na mbili na Geneva 4 kushindwa kuzaa matunda mazuri kutokana na ukwamishaji wa nchi kama Uturuki na kuweko mizozo na mivutano mingi ndani ya wapinzani wa Syria, mazungumzo ya Astana tatu yaliyopangwa kufanyika juzi tarehe 15 Machi nayo yalishindwa kutokana na wapinzani kukataa kushiriki. Mara baada ya ukwamishaji wao huo, magaidi nchini Syria wameanzisha wimbi jipya la mashambulizi ya mabomu katika maeneo ya raia ili kuishinikiza serikali ya Damascus.
Tunaweza kusema kuwa, mazungumzo na vitendo vya kigaidi ni pande mbili za sarafu ya mgogoro wa Syria na kila pale mazungumzo yanaposhindwa kuzaa matunda, nchi hiyo ya Kiarabu hukumbwa na mashambulizi makubwa ya kigaidi. Katika miezi ya hivi karibuni, magaidi walikumbwa na kibuhuti kikubwa hasa baada ya pigo walilolipata huko Halab, lakini Uturuki na Marekani zimekwamisha kwamisha mambo katika mazungumzo ya pande tatu ya Astana na Geneva 4 ili kuyarejeshea nguvu magenge ya kigaidi. Hata Staffan de Mistura, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria amesema kuwa, lengo la miripuko ya kigaidi ya hivi karibuni nchini Syria ni kuzuia kufanikiwa mazungumzo ya amani na kuvuruga juhudi za kimataifa za kutatua mgogoro wa nchi hiyo.
Kwa kuzingatia yote hayo tunaweza kusema kuwa, miripuko ya siku za hivi karibuni huko Damascus Syria ni moja na natija kuu za kushindwa mazungumzo ya pande tatu ya Astana na Geneva ambayo katika hatua zake za awali ilikuwa ni kusimamisha vita baina ya pande zinazoshiriki kwenye mazungumzo hayo. Suala la kusimamisha mapigano limekuwa likisisitizwa mno katika mazungumzo ya amani ya Syria kiasi kwamba hata katika mazungumzo ya Astana 3 ambapo wapinzani wenye silaha wa Syria walikataa kushiriki, wajumbe kutoka Russia, Iran na Uturuki walisisitizia udharura wa kuimarishwa usitishaji mapigano nchini humo.
Tunapotilia maanani yote hayo tutaona kuwa, hakuna matumaini yoyote ya kufanikiwa mazungumzo ya Geneva 5 yanayotarajiwa kufanyika siku chache zijazo yaani tarehe 23 Machi na wala mazungumzo ya Astana 4 ambayo yamepangwa kufanyika tarehe tatu na nne Mei mwaka huu. Na sababu ni kuwa, kinyume na msimamo wa Russia, Iran na Syria, wahusika wengine kama vile Uturuki na Marekani pamoja na wapinzani wanaona kuwa kumalizika mgogoro wa Syria hivi sasa ni kwa madhara yao, hivyo wanafanya kila njia ili kukwamisha juhudi za kuutafutia ufumbuzi wa kudumu mgogoro huo.