Misri: Hatujatuma askari wetu nchini Yemen
Serikali ya Misri imekadhibisha madai yaliyotolewa na Msemaji wa Muungano wa Kichokozi wa Saudia dhidi ya Yemen kwamba Cairo imetuma askari wake nchini Yemen.
Awali Ahmad Asiri, Msemaji wa Muungano wa Kichokozi wa Saudia dhidi ya Yemen alidai kuwa Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri ametoa amri ya kutumwa askari elfu 40 wa nchi yake kwa ajili ya kushiriki katika vita vya ardhini na vya kiuchokozi huyo Yemen.
Hata hivyo Shirika la Habari la Russia al-Yaum, limemnukuu afisa wa ngazi ya juu serikalini ambaye hakutaka kutaja jina lake akisema kuwa, matamshi ya Ahmad Asiri hayana msingi wowote. Amesema kuwa, kutumwa askari wa Misri kwenda nje ya mipaka ya nchi hiyo kwa ajili ya kushiriki vita, kuna sheria zake maalumu na sio kukurupuka tu. Itakumbukwa kuwa, utawala wa Aal-Saud kwa kushirikiana na Marekani, Uingereza, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi, ilianzisha mashambulizi ya kila upande dhidi ya Yemen mwezi Machi mwaka 2015 kwa lengo la kutaka kumrejesha madarakani kibaraka wake Abdrabbuh Mansur Hadi, rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu na kutoroka nchi.
Hata hivyo licha ya kulisababishia hasara kubwa za mali na roho taifa hilo masikini la Kiarabu, utawala huo na washirika wake umeshindwa kufikia malengo yake machafu kutokana na msimamo imara wa jeshi la Yemen kwa kushirikiana na Harakati ya Kiislamu ya Answarullah ya nchi hiyo.