Taliban waua makumi ya askari wa Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i28084-taliban_waua_makumi_ya_askari_wa_afghanistan
Zaidi ya askari 50 wa Afghanistan wameuawa katika shambulio lililofanywa na wapiganaji wa kundi la kitakfiri la Taliban dhidi ya kambi muhimu ya jeshi la nchi hiyo huko kaskazini mwa Afghanistan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 21, 2017 23:13 UTC
  • Taliban waua makumi ya askari wa Afghanistan

Zaidi ya askari 50 wa Afghanistan wameuawa katika shambulio lililofanywa na wapiganaji wa kundi la kitakfiri la Taliban dhidi ya kambi muhimu ya jeshi la nchi hiyo huko kaskazini mwa Afghanistan.

Msemaji wa jeshi la Marekani, Kanali John Thomas, amesema kuwa askari wapatao 50 wa Afghanistan wameuawa katika shambulizi hilo lililolenga msikiti na ukumbi wa chakula.

Duru za habari za Afghanistan zimeripoti kuwa, mapigano makali yalisikika jana Ijumaa katika kambi ya jeshi la taifa la Afghanistan katika mji wa Mazar-e-Sharif ulioko kwenye mkoa wa Balkh na kwamba zaidi ya askari 50 wameuawa.

Habari zinasema wapiganaji wa kundi la Taliban waliingia katika kambi hiyo wakiwa na sare za jeshi la Afghanistan wakati wa Swala ya Ijumaa na kufanya shambulizi hilo.

Magaidi wa kundi la Taliban, Afghanistan

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Afghanistan, Daulat Waziri, amesema kuwa, wanachama wa kundi hilo la kigaidi walivamia kambi hiyo kwa gari na kuanza kuwafyatulia risasi wanajeshi waliokuwa wakitekeleza Swala ya Ijumaa katika msikiti wa kambi hiyo. Amesema wanachama 5 wa kundi la Taliban akiwemo mmoja aliyekuwa amejifunga mada za milipuko wameuawa katika hujuma hiyo.