Juhudi zisizo na matunda za Israel za kusambaratisha Intifadha ya Quds
Baada ya juhudi za Israel za kusambaratisha Intifadha ya Quds kushindwa, Kamati ya Usalama ya utawala huo ghasibu sasa imechukua maamuzi mapya yanayolenga kuikandamiza Intifadha hiyo.
Kuongeza kasi ya ubomoaji wa nyumba za watekelezaji wa operesheni za muqawama na kutolewa hukumu za kimahakama katika uwanja huo ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Kamati ya Usalama ya Israel ambazo utekelezwaji wake unalenga kuitokomeza Intifadha ya Quds. Aidha kamati hiyo imechukua uamuzi wa kuzinyima haki ya kufanya kazi, familia za watekelezaji wa operesheni za muqawama dhidi ya Israel na kuvifungia pia baadhi ya vyombo vya habari. Katika uga huo, Ijumaa ya jana wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel walifunga ofisi ya Kanali ya Televisheni ya Palestina ya al-Yaum huko katika Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan na kumtia mbaroni mkuu wa ofisi hiyo pamoja na wafanyakazi wake. Hatua hiyo ya Israel imekabiliwa na radiamali ya Wapalestina ambao wamelaani vikali kitendo hicho.
Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina imelaani hatua hiyo ya wanajeshi wa Israel na kutangaza kuwa, uvamizi katika ofisi hiyo umefanyika katika fremu ya hatua za kigaidi za jeshi na walowezi wa Kiyahudi dhidi ya taifa la Palestina.
Kwa upande wake Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imelaani uvamizi na kufungwa ofisi ya Kanali ya Televisheni ya Palestina ya al-Yaum na kutangaza kuwa, kitendo hicho kinalenga kuzima sauti ya ukweli na wakati huo huo kusitisha Intifadha. Kamati za muqawama za Palestina nazo zimelaani hatua hiyo ya Israel na kueleza kuwa, shambulio dhidi ya Ofisi ya Kanali ya Televisheni ya Palestina ya al-Yaum linaonesha kuwa, utawala ghasibu wa Israel hauwezi kustahamili chombo huru cha habari, chenye kufungamana na kadhia ya Palestina na ambacho kinaliunga mkono taifa madhulumu la Palestina.
Kadhalika Kituo Huru cha Habari cha Gaza kimekosoa vikali hatua ya Israel ya kuifunga ofisi ya Televisheni ya al-Yaum na kuzitaka asasi zote za kisheria za Kiarabu na za kimataifa, wanaharakati wa kutetea uhuru wa vyombo vya habari na waandishi wa habari kuonesha radiamali kwa kitendo hicho cha Israel. Walowezi wa Kiyahudi nao ambao daima wamekuwa wakitenda jinai nyingi dhidi ya Wapalestina wakipata himaya ya wanajeshi wa Israel wamechoma moto nyumba ya Mpalestina kusini mwa Bait Lahm katika Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan.
Israel inachukua hatua za kukabiliana na Intifadha katika hali ambayo, Wapalestina wanaendelea na muqawama na mapambano yao sambamba na maandamano katika maeneo mablimbali ya Palestina hali inayosisitiza kudumishwa Intifadha dhidi ya Quds.
Tangu Oktoba mwaka jana maeneo mbalimbali ya Palestina yamekuwa yakishuhudia malalamiko dhidi ya siasa za kivamizi na njama za utawala dhalimu wa Israel za kutaka kubadilisha utambulisho wa Baytul Muqaddas, harakati ambazo zimetambulika kama Intifadha ya Quds. Tangu kuanza Intifadha hiyo Oktoba mwaka jana hadi sasa zaidi ya Wapalestina 20 wameuawa shahidi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Ukanda wa Gaza na Baaytul Muqaddas.
Ukweli wa mambo ni kuwa, kuendelea Intifadha ya Quds ni ithibati tosha ya kugonga mwamba njama zote za Wazayuni za kutaka kuisambaratisha Intifadha hiyo.