Syria: Sababu ya kutokea mashambulio ya kigaidi mjini Tehran hii hapa
(last modified Wed, 14 Jun 2017 15:36:11 GMT )
Jun 14, 2017 15:36 UTC
  • Sattam Jadaan Al-Dandah, balozi wa Syria nchini Iraq akizungumza na waandishi wa habari
    Sattam Jadaan Al-Dandah, balozi wa Syria nchini Iraq akizungumza na waandishi wa habari

Balozi wa Syria nchini Iraq amesema kuwa, sababu kuu ya kutokea mashambulizi ya kigaidi mjini Tehran, ni kutokana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa nchi pekee iliyosimama kikweli na wananchi na serikali za Iraq na Syria kupambana na magenge ya kigaidi yaliyozivamia nchini hizo.

Sattam Jadaan Al-Dandah, amenukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari akilaani vikali mashambulizi mawili ya kigaidi yaliyotokea mjini Tehran Jumatano iliyopita na kusema kuwa, magenge ya kitakfiri yameilenga Tehran kutokana na msimamo usiotetereka wa Iran katika kushirikiana na nchi za Syria na Iraq kupambana na ugaidi.

Sehemu alipojiripua mmoja wa magaidi waliovamia Haram ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) Jumatano, Juni 7, 2017

 

Jumatano ya tarehe 7 mwezi huu wa Juni, magaidi wa genge la Daesh walishambulia jengo la kiidara la Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na Haram ya Imam Khomeini MA mjini Tehran.

Watu 17 waliuawa shahidi na karibu 50 wengine kujeruhiwa kwenye mashambulio hayo. Hata hivyo maafisa usalama wa Iran walizima haraka mashambulizi hayo kwa kuwaangamiza magaidi wote walioshiriki moja kwa moja kwenye ugaidi huo na kuwatia mbaroni wengine wengi waliohusika na mashambulizi hayo.

Balozi wa Syria nchini Iraq amegusia pia siasa za Marekani kuhusiana na matukio ya eneo hilo na kusema kwamba, tangu alipoingia madarakani rais wa Marekani, Donald Trump, machafuko na ukosefu wa usalama umeongezeka sana katika eneo hili la magharibi mwa Asia.