Jun 18, 2017 13:36 UTC
  • Saudia na Israel zafanya mazungumzo kuhusu makubaliano ya kibiashara

Gazeti la The Times la Uingereza limefichua kuwa Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni wa Israel zinafanya mazungumzo juu ya kile kinachotajwa kuwa mabadilishano rasmi ya kihistoria ya kibiashara.

Gazeti hilo limenukuu vyanzo vya habari vya Marekani na nchi za Kiarabu vikisema kuwa, katika hatua ya kwanza ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara wa pande mbili, Riyadh itaruhusu ndege za shirika la utawala haramu wa Israel la El Al kutumia anga yake.

Kadhalika inaarifiwa kuwa utawala wa Aal-Saudi umeafiki kuwaruhusu wafanyabiashara na wajasiriamali wa Israel kuwekeza rasmi ndani ya ardhi yake.

Duru nyingine za habari zinasema kuwa, makubaliano ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Saudia na Israel ni jitihada tu za Ikulu ya Marekani ya White House za kutaka kuonyesha kuwa safari ya Rais Donald Trump wa Marekani huko Riyadh na Tel Aviv imezaa matunda.

Kuimarika uhusiano wa Saudia na Israel

Itakumbukwa kuwa, Rais Donald Trump wa Marekani na Mfalme Salman wa Saudia hivi karibuni wakiwa mjini Riyadh walitia saini mkataba wa mauzo ya silaha wenye thamani ya dola bilioni 110 za Marekani.

Kadhalika Trump alipokea mkufu wa dhahabu na zawadi nyingine zenye thamani ya dola bilioni 1.2 za Marekani kutoka kwa Mfalme Salman wakati wa safari yake hiyo ya kwanza nje ya nchi mjini Riyadh tangu aapishwe kuwa Rais wa Marekani.

Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni Saudia ilizochochea nchi kadhaa za Kiarabu na Kiafrika kukata uhusiano wao wa kidiplomasia na kibiashara na Qatar, kwa madai bandia kuwa Doha inaunga mkono na kufadhili magenge ya kigaidi.

 

Tags